Sep 12, 2013

Mikataba yaitafuna TAZARA


Wakati Wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (Tazara) wakimaliza mgomo, uongozi wa mamlaka hiyo umetuhumiwa kuingia makubaliano ya mkataba mbovu unaochangia matatizo yaliyopo.

Tuhuma hizo zimetokana na makubaliano ya mkataba wa kibiashara uliofanyika mwaka jana kati ya Shirika la Reli Zambia (ZNL) na Tazara ili kubadilishana mizigo ya shaba itokayo Bandari ya Kitwe mpaka Bandari ya Kapirimposhi kwa madai ya ubovu wa njia za reli.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya mamlaka hiyo kilieleza kuwa, kutokana na makubaliano hayo, ZNL imekuwa ikichukua faida ya asilimia 40 ya mapato yaingiayo Tazara. 

“Tazara inaingiza mapato mengi, lakini makubaliano hayo yanaonekana kuinyonya, kwa sasa inabakiwa na faida ya asilimia 60 kwa ajili ya kuendeshea shughuli zake, hivyo bajeti ya mshahara inabakia kidogo,” kilieleza.

Kiliongeza kuwa mbali ya kulalamika mkataba huo uvunjwe, utaratibu huo bado unaendelea kutekelezwa na haifahamiki utasitishwa lini.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Tazara (Trawu), Musa Kalala alikiri kuwepo mkataba huo na kwamba makubaliano yalifanyika ndani ya bodi.

Naye Msemaji wa mamlaka hiyo, Conrad Simuchile alikiri kuwepo makubaliano hayo, huku akikanusha tuhuma hizo kwa maelezo ya sababu zilizochangia ZNL na Tazara kuingia makubaliano.

“Kwanza njia ya reli ni mbovu na treni ya Tazara ni nzito kwa hivyo haiwezi kupita katika reli inayoanzia Kapirimposhi mpaka Kitwe kwa treni, hivyo ndiyo sababu ya kuingia kwa makubaliano hayo,” alisema.
 

0 comments:

Post a Comment