Sep 26, 2013

Kuuliwa kwa Samantha ni Kizungumkuti



Utata umezuka kuhusu taarifa za kuuawa kwa gaidi mwanamke raia wa Uingereza, Samantha Lewthwaite (29) anayedaiwa kuongoza mashambulio ya magaidi wa kundi la Al Shabab mjini Nairobi, Kenya. Utata huo unakuja baada ya kuonekana baadhi ya picha kwenye mitandao zikimuonyesha mwanamke huyo akitoka nje ya Jengo la Biashara la Westgate akijifanya kuwaokoa baadhi ya majeruhi wa shambulio hiyo.

Awali taarifa zilisema kuwa mwanamke huyo aliuawa katika harakati za kutupiana risasi kati ya magaidi wa Al Shabab na askari wa Kenya.


Gazeti la Daily Mail la Uingereza juzi lilikariri vyanzo vyake ndani ya jeshi na mfumo wa usalama nchini Kenya vikithibitisha kuwa nwanamke huyo alikuwa miongoni mwa magaidi waliouawa katika tukio hilo.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohammed, katika mahojiano yake na kituo cha habari cha PBS, hakusema iwapo mwanamke huyo alikuwa ameuawa lakini alithibitisha kuwa miongoni mwa magaidi waliovamia Westgate ni mwanamke wa Uingereza, ambaye hakumtaja jina.

Hatua hiyo iliibua tetesi kwenye vyombo vya habari vya Kenya ambavyo vilimtaja mwanamke huyo kuwa ni Samantha.

Kauli ya Waziri huyo ilionekana kupingana na ile iliyotolewa awali na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Kenya, ambaye alisema magaidi wote waliovamia kituo hiocho walikuwa wanaume na kwamba huenda baadhi yao walivalia mavazi ya kike.

0 comments:

Post a Comment