Sep 11, 2013

Katiba mpya kutumika baada ya uchaguzi wa 2015



SASA ni wazi kwamba, kuna wingu la mashaka limetanda juu ya uwezekano wa Katiba Mpya kutumika kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kutokana na kauli pamoja na mwenendo wenye mwelekeo wa kuipinga ambao umeendelea kushuhudiwa tena katika siku za hivi karibuni. Jana na juzi kwa nyakati tofauti, Serikali pamoja na Jukwaa la Katiba limetoa kauli yenye mwelekeo huo huo.

Wakati Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, akisema upo uwezekano wa kutumia Katiba iliyopo sasa iwapo Katiba Mpya itakuwa haijakamilika katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba naye ametoa kauli inayofanana na hiyo.


Kwa upande wake, Chikawe alitoa kauli hiyo juzi jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na kituo cha runinga cha ITV.

Alisema endapo Katiba Mpya haitapatikana, uwezekano wa kutumia iliyopo sasa katika uchaguzi mkuu wa 2015 ni mkubwa, kwa sababu imekamilika na imeweza kuivusha Tanzania katika kipindi cha miaka 50.

Kwa upande wake Kibamba, alisema kuna haja ya kuifanyia marekebisho Katiba iliyopo sasa, ili iweze kutumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Kibamba alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo alielezea wasiwasi wake juu ya kasi ya mchakato wa Katiba Mpya inavyokwenda.

Alisema anajua wazi kwamba endapo Katiba iliyopo sasa itafanyiwa marekebisho ambayo yataipa uwezo Tume ya Uchaguzi kuwa huru, basi itaweza kusimamia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 bila matatizo, hivyo kumpa nafasi kiongozi ajaye kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya kwa minajili ya kupata Katiba bora.

“Mchakato wa Katiba unatakiwa kuendeshwa kwa mwendo wa kinyonga, lakini kwa kasi hii kweli napata wasiwasi mkubwa....mwakani ni uchaguzi wa Serikali za mitaa na mwaka 2015 tunafanya uchaguzi mkuu, sidhani kama Katiba hii itakuwa imekamilika zaidi ya kulipuliwa,” alisema Kibamba.

Pia alisema kuwa anapinga vikali Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya pili ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, kwa kile alichodai kuwa umepitishwa kwa mizengwe huku ukiwa na upungufu mwingi.

Mbali na hayo, awali Waziri Chikawe wakati akizungumzia hoja yake hiyo ya Katiba, pia alikanusha juu ya kile kinachodaiwa kuwa Serikali imekuwa ikiingilia mfumo wa ukusanyaji wa maoni ya Katiba kupitia kwa viongozi wake kama vile wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa, jambo ambalo si kweli.

“Kitendo cha wakuu wa wilaya kuungana na kusema wanaunga mkono Serikali mbili, kisitafsiriwe kuwa Serikali ndiyo imewatuma, kwa sababu wale kweli ni wawakilishi wa Serikali lakini hilo halina mantiki kwamba tumewaagiza kwani na wao pia wanamaoni yao kama watu wengine.

“Upande wa Serikali ni sera yetu kuhakikisha tunamwezesha Jaji Warioba, hatuwezi kumwingilia wala hatujawahi kumwingilia, bajeti tunawatafutia, wakuu wa wilaya na mikoa kutoa misimamo ya Serikali mbili hiyo ni misimamo yao, na msimamo wa Serikali ni kwamba hatujawatuma kwani Serikali ndiyo iliyouanzisha mchakato huo,” alisema.

Aidha akizungumzia kitendo cha vyama vya siasa kuingilia mchakato huo, Chikawe alisema hilo ni jambo ambalo haliepukiki.

“Kama kuna rushwa kwenye mchakato huu kwa kweli tunaulaani, lakini pamoja na hayo, kimsingi tunapaswa kufahamu ile ‘document’ ya Katiba ni ya kisiasa, hivyo lazima vyama vya siasa viingilie kwani wale ni sawa na mechi ya mpira umwekee refarii wa kikapu, wataingia sana tu hao wanasiasa,” alisema.

Akizungumzia matumizi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilipewa Sh bilioni 38 mwaka jana na mwaka huu vilevile, Chikawe aliitetea akisema haitumii fedha ovyo kama watu wanavyodai na kwamba hakuna ubadhirifu wowote uliotokea.

Mbali na hilo, Chikawe pia alizungumzia kitendo cha Tume kushindwa kuweka wazi kuhusu kufuta adhabu ya kifo, kwa sababu ni adhabu ambayo haijatekelezwa kwa muda wa miaka 18.

Alisema kwa upande wake, alipendekeza ifutwe na adhabu mbadala iwe kifungo cha maisha, kwa sababu mtu akinyongwa hapewi muda wa kujirekebisha, pia huwa kunatokea makosa kwa kunyonga watu ambao si wakosaji.

0 comments:

Post a Comment