Mar 10, 2016

Israel ni hatari kwa amani na usalama wa dunia

Iran: Israel ni hatari kwa amani na usalama wa dunia
Mwakilishi wa Iran katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) amesema vichwa vya silaha za nyuklia vinavyomilikiwa na utawala haramu wa Israel ni tishio kuu kwa amani na usalama wa dunia. 
 
Reza Najafi, Balozi wa Iran katika wakala wa IAEA ameeleza wasi wasi wake kuhusu hatua ya Israel kutoruhusu wakaguzi wa wakala huo wa nishati ya atomiki kuchunguza hifadhi zake haramu na za siri zenye silaha hizo za maangamizi. 

Mwakilishi wa Iran katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki amekariri kuwa, ni kichekesho namna utawala wa Kizayuni wa Israel unavyoendelea kumiliki silaha hizo hatari kwa upande mmoja, na kuingiwa na kiwewe kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani kwa upande mwingine. 

Reza Najafi aliyasema hayo jana Jumatano katika barua rasmi kwa Yukiwa Amano, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA na kuongeza kuwa, ‘machozi ya mamba' ya utawala huo haramu dhidi ya miradi ya nyuklia ya Iran hayawezi kuficha ukweli kuwa unamiliki silaha za nyuklia, ambazo ni tishio kwa usalama na amani ya eneo na dunia kwa jumla. 

Takwimu zisizo rasmi zinaonyesha kuwa Israel ina zaidi ya vichwa 200 vya silaha za nyuklia kwenye hifadhi zake.

0 comments:

Post a Comment