Usama Hamdan, Mkuu wa Mahusiano ya
Nje wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema
mapendekezo yaliyotolewa na Misri katika mazungumzo ya Cairo hayakidhi
matakwa ya Wapalestina.
Kiongozi huyo mwandamizi wa HAMAS amesisitiza
kuwa utawala wa Kizayuni hauna chaguo jengine ghairi ya moja kati ya
mawili; ima kukubali masharti ya Palestina au kukabiliana na vita vya
msuguano vya muda mrefu.
Hamdan, ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa
kuiunga mkono Gaza uliofanyika mjini Khartoum, Sudan, ameongeza kuwa
kuna mikakati inayotekelezwa katika mazungumzo ya usitishaji vita ya
Cairo kwa lengo la kuusamabaratisha umoja katika ujumbe wa Wapalestina
katika mazungumzo hayo.
Katika upande mwengine Azzam al Ahmad, mkuu wa
Palestina katika mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana na utawala wa Kizayuni
wa Israel amesisitiza kwamba haitowezekana viongozi wa Palestina
kukubali maafikiano yoyote ambayo hayatodhamini haki na malengo ya taifa
la Palestina.
Hii ni katika hali ambayo serikali ya Misri imezikabidhi
pande mbili za Palestina na Israel mapendekezo yake rasmi ya usitishaji
vita huko Gaza na kuutaka kila upande utoe msimamo wake kuhusiana na
mapendekezo hayo.
Hivi sasa usitishaji vita wa muda wa siku tano
unaendelea huko Gaza ambao ulianza kutekelezwa siku ya Alkhamisi
iliyopita.
0 comments:
Post a Comment