Uamuzi huo wa Ikulu umetolewa jijini Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alipokuwa akizungumza na MTANZANIA.
Alisema Bunge Maalumu la Katiba lilianzishwa na linaendeshwa kwa mujibu wa sheria ambayo haina kifungu chochote kinachomtaka rais kulisitisha.
“Hakuna mpango huo kwa hivi sasa, Bunge Maalumu la Katiba limeanzishwa na linaendeshwa kwa mujibu wa sheria. Sheria hiyo haina kifungu cha rais kulisitisha,” alisema.
Sitta awashangaa
Akizungumzia kauli hiyo ya Ukawa, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, alisema Bunge huendeshwa kwa mujibu wa sheria, na wanaosema lisitishwe hawana hoja kwani kila siku wamekuwa wakibadilika.
“Bunge hapa linaendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria, hawa watu kila siku wana hoja mpya,” alisema Sitta.
Alisema kuwa vitisho wanavyovitoa havimshtui.
“Kazi yao ni kulishambulia Bunge Maalumu tu, wanasema gharama, hata uchaguzi una gharama zake,” alisema.
Awali akizungumza na jumuiya ya wafugaji waliotembelea ofisini kwake mjini Dodoma na kuwasilisha mapendekezo wanayotaka yaingizwe kwenye Katiba mpya, Sitta alisema waliotoka nje ya Bunge hilo na sasa hivi wanapiga kelele wakitaka lisitishwe, hawawatakii Watanzania mema.
“Walioko hapa wanatosha kabisa kuendelea na mchakato mpaka mwisho,” alisema Sitta.
Juzi, Ukawa walitoa masharti manne kwa Rais Kikwete, ikiwamo kumtaka asitishe shughuli za Bunge Maalumu la Katiba ili wajumbe wake wasiendelee kufuja fedha za Watanzania.
Tamko hilo lililotolewa na wenyeviti wa vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na Chadema, vinavyounda umoja huo.
Hata hivyo, tamko lao halikumpa Kikwete siku ya mwisho ya kutekeleza agizo lao.
Mbali na hatua hiyo, pia wamemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalumu juu ya matumizi ya fedha za Bunge hilo, kuanzia Bunge la Bajeti lililopita, wakidai wamebaini kuwapo ufisadi na kukosekana maelezo sahihi.
0 comments:
Post a Comment