Aug 14, 2014

Idadi ya wakimbizi wa ndani Iraq imefika milioni 1.5


Jamii ya Yezidi wamelala kivulini baada ya kukimbia Sinjar.

Siku Moja baada ya Umoja wa Mataifa kutangaza kwamba tatizo la kibinadamu Iraq limefikia ngazi ya juu kabisa ya dharura, Ujumbe wa Umoja huo nchini Iraq, UNAMI, umeeleza kwamba idadi ya wakimbizi inazidi kuongezeka kila siku.

Kwa mujibu wa msemaji wa UNAMI, Eliana Naaba, hali mbaya ya kibinadamu nchini Iraq tayari imekithiri, na idadi ya wakimbizi wa ndani inaongezeka kila yanapotokea mashambulizi mengine. 

Amesema kwamba tayari idadi hiyo imefika milioni moja na nusu, na kuamua kuitisha ngazi ya tatu ya dharura kutarahisisha usambazaji na usafirishaji wa misaada pamoja na mambo ya urasimu.

Alipoongea na Redio ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, ameeleza kwamba watu 1,000 tu wamebaki na kunaswa kwenye mlima wa Sinjar, wengine wakiwa wamepata njia ya kujinasua.

Ameongeza kuwa mahitaji ya wakimbizi hao ni mengi sana:


" Mahitaji yao ni ya kila aina. Unapswa kuelewa kwamba watu hao wamekimbia makwao wakiwa na nguo zao tu walizovaa. 

Kwa hiyo wanahitaji kila kitu: chakula, maji, makazi, usafi, dawa, vyombo vya kupikia, blanketi, kila kitu. Wamekuja na nguo zao tu walizovaa. 

Mahitaji yao ni mengi mno"
Ngazi ya tatu ya udharura ndiyo ngazi ya mwisho katika matatizo ya kibinadamu na kwa sasa hivi, ngazi hiyo imefikiwa kwenye mizozo ya Syria, Sudan Kusini na Afrika ya Kati

0 comments:

Post a Comment