Mufti Mkuu wa Misri amesema kuwa
vitendo vinavyofanywa na kundi la Daesh vinapingana na thamani za
kibinadamu na Kiislamu na kwamba kundi hilo ni genge la kigaidi ambalo
haliwezi kutambuliwa kuwa ni dola la Kiislamu.
Mufti Mkuu wa Misri Shauqi Allam ametoa
wito wa kuwepo ushirikiano wa kikanda na kimataifa kwa shabaha ya
kukabiliana na vitendo vya kundi la Daesh na makundi mengine ya kigaidi.
Amesema kuwa kundi la kigaidi la Daesh mbali na kukanyaga thamani za
Kiislamu na malengo aali ya sheria yaliyowekwa na dini ya Uislamu,
limekiuka pia thamani za kibinadamu zinazowakutanisha pamoja wanadamu
wote.
Mufti Mkuu wa Misri amesema Daesh na
makundi mengine ya kigaidi ni hatari kubwa kwa Uislamu na Waislamu na
kuongeza kuwa, makundi hayo yanachafua sura ya Uislamu kama ambavyo
yanamwaga damu za watu wasio na hatia na kueneza ufuska na ufisadi.
Ameongeza kuwa vitendo vya kundi hilo vinadhoofisha mataifa na nchi za
Kiislamu na kutayarisha uwanja mzuri wa maadui kuingilia mambo ya ndani
ya Waislamu kwa kisingizio cha vita dhidi ya ugaidi.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa Idara ya
Fatuwa ya Misri (Darul Iftaa) imezitaja jinai zinazofanywa na kundi la
Daesh huko Iraq kuwa ni jinai dhidi ya binadamu na kwamba hatua za kundi
hilo zinapingana na mafundisho ya Uislamu.
Kituo hicho cha juu cha
kidini nchini Misri pia kimekuwa kikisisitiza juu ya udharura wa
kupambana na kundi hilo la kigaidi la Daesh na makundi mengine yenye
misimamo ya kufurutu mipaka.
0 comments:
Post a Comment