Aug 14, 2014

Baraza la Usalama latoa wito wa kuundwa haraka serikali nchini Iraq


Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa wito wa kuundwa serikali mpya nchini Iraq haraka iwezekanavyo na kuzitaka pande mbalimbali kutulia na kuheshimu mchakato wa kisiasa unaoongozwa na katiba. 

Taarifa iliyotolewa na baraza hilo inasema limetiwa moyo na uamuzi wa rais wa Iraq Fuad Masum wa kumteua waziri mkuu mpya, na kwamba hiyo ni hatua muhimu katika kuunda serikali inayowakilisha pande zote za Iraq na ambayo itachangia kutafuta utatuzi wa kudumu na wenye manufaa kwa changamoto za nchi hiyo. 

Baraza pia limemtaka waziri mkuu mteule Bw Haider al-Abadi, kuharakisha kuunda serikali hiyo. Bw. Al-Abadi, mbunge kutoka chama cha kiislamu cha Shia kinachoongozwa na waziri mkuu Nuri al-Malik, ana siku 30 za kuunda serikali mpya. 

Umoja wa Mataifa pia umelaani vikali vitendo vya kinyama vya unyanyasaji wa kingono na ubakaji ambavyo vinafanywa na kundi la ISIS dhidi ya wanawake, wasichana na wavulana katika maeneo wanayoyadhibiti ya makabila madogo ya Iraq. 
 
Habari nyingine zinasema rais François Hollande wa Ufaransa jana alizungumza na Waziri Mkuu wa Uingereza Bw. David Cameron kwa njia ya simu kuhusu hali ya Iraq, na kukubaliana kusafirisha misaada ya kibinadamu kwa watu wa Iraq waliopo hatarini, na kutoa silaha kwa wanajeshi watakaotoa ombi husika. 

Zaidi ya hayo, rais Hollande ametangaza kuwa Ufaransa itatuma silaha kwenye eneo linalojitawala la waKurd ndani ya saa kadhaa zijazo, ili kuimarisha uwezo wake wa kupambana na kundi la ISIS.

0 comments:

Post a Comment