Jul 28, 2014

SERIKALI YAIFUNGA HOSPITALI IMTU

Serikali yaifunga hospitali IMTU

HOSPITALI ya Chuo cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU)
kinachohusishwa na utupaji wa viungo vya binadamu mithili ya takataka, Imefungiwa kwa muda usiojulikana baada ya kugundulika kutokidhi viwango na maadili ya utoaji huduma za hospitali nchini.
Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imechukua jukumu la kuifungia hospitali hiyo baada ya kufanya ukaguzi wa kushitukiza na kubaini uwepo wa mapungufu kadhaa.

Mapungufu yaliyobainika kuwepo katika hospitali hiyo ni pamoja na kutokuwa na wauguzi wa kutosha, kutokuwa na vifaa vya kutosha ikiwemo kifaa cha kuchomea taka ngumu, kuchanganya dawa zilizokwisha muda na ambazo hazijaisha muda wake na pia wauguzi kufanya kazi ambazo si za kwao.

Akizungumza wakati wa kufunga hospitali hiyo, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Dk Gunini Kamba alisema, hospitali hiyo inastahili kufungiwa kutokana na kutokidhi viwango hivyo.

“Baada ya kufanya ukaguzi wa kushitukiza tumebaini kuwepo kwa mapungufu haya, kwa hiyo tunaifungia hospitali hii mpaka pale watakaporekebisha,” alisema Dk Kamba.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Profesa Yassin Mgonda alikiri kuwepo kwa mapungufu hayo ambayo aliahidi kuyafanyia kazi. Hata hivyo, Profesa Mgonda aliiomba Manispaa na Wizara ya Afya kuangalia adhabu hiyo waliyoitoa.

Baadhi ya wagonjwa waliokuwa hospitalini hapo wakipata huduma walishtushwa na kusikitishwa na kitendo hicho, lakini walikipongeza na kutaka kuwa endelevu.
Mmoja kati ya wagonjwa hao aliyejitambulisha kwa jina la Neema Kiwalo alisema, ukaguzi huo unatakiwa kuwa endelevu ili kuendelea kufichua madudu yaliyopo katika hospitali mbalimbali nchini.

Aidha, Msemaji Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja alisema, endapo hospitali hiyo watatimiza masharti waliyopewa na Mganga Mkuu wa Manispaa wao kama wizara watafanya ukaguzi kuona kama wamekamilisha.

Alisema ikiwa watakuwa wamerekebisha kasoro hizo zilizopelekea kufungiwa hospitali hiyo itaruhusiwa kutoa huduma zake kama kawaida.

Hospitali hiyo imefungiwa wakati kukiwa kuna sakata linalolihusisha chuo chake, kinachodaiwa kutupa viungo vya binadamu jalalani.

Katika sakata hilo lililovuta hisia za watu na kuzua mjadala mitaani, katika vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii, watu wanane wakiwemo madaktari wa IMTU, walikamatwa na Polisi kwa mahojiano wakituhumiwa kuhusika katika utupaji viungo vya binadamu jalalani.

Serikali wakati ikiendelea kuchunguza tukio hilo ikiwemo kuunda tume nyingine ya watu 15 chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kujiridhisha kabla ya hatua kuchukuliwa iliyopewa siku saba kukamilisha kazi yake, tume hiyo imeundwa kukiwa na tume nyingine iliyoundwa na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Tume iliyoundwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imejielekeza kuja na majibu kadhaa, ikiwa ni pamoja na kufahamu idadi kamili ya watu wenye viungo hivyo.
Ikiwa na watu saba akiwemo Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume hiyo itakuja na majibu yanayofafanua viungo hivyo ni vya muda gani na zilitumika kemikali gani kuvikausha. Pia, jopo hilo litabaini kama ipo sheria na ni ipi inavunjwa.

Wataalamu hao wanalenga kubaini, pia kama upo uzembe katika kulinda viungo vya binadamu na vinapatikanaje kwa ajili ya mazoezi.


Kwa mujibu wa Polisi, mifuko ipatayo 85 yenye vichwa, miguu, mikono, moyo, mapafu, vifua na mifupa ya aina mbalimbali ya binadamu, ilikutwa maeneo ya bonde la Mbweni Mpiji eneo la Bunju jijini Dar es Salaam.

0 comments:

Post a Comment