Jul 30, 2014

80 wafariki dunia wakisherehekea Idi, Guinea Conakry

Watu wasiopungua 80 wanaripotiwa kufariki dunia katika msongamano na kukanyagana kwa watu waliokuwa katika tamasha la Sikukuu ya Idul Fitri katika pwani ya mji mkuu wa Guinea, Conakry. 

Makumi ya watu wengine wamejeruhiwa katika tukio hilo lililotokea jana Jumanne.

Msongamano na kukanyagana huko kwa watu kulitokea wakati walipokuwa katika tamasha ya muziki kwenye eneo la Ratoma, iliyofanyika kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu ya Idul Fitri ya kukamilisha mfungo wa mwezi wa Ramadhani.


Maafa hayo yametokea katika kipindi cha sasa ambapo nchi ya Guinea Conakry inakabiliana na mfumuko wa ugonjwa wa Ebola unaoenea kwa kasi katika nchi za magharibi mwa Afrika.


Ofisi ya Rais wa Guinea Conakry imetangaza wiki nzima ya maombolezo ya kitaifa ya maafa hayo. 


Vyombo vya usalama vya Guinea vimeanza uchunguzi wa kubaini mazingira na chanzo cha maafa hayo.

0 comments:

Post a Comment