Jun 27, 2014

Al Qaida washambulia uwanja wa ndege Yemen



Habari kutoka Yemen zinasema kuwa, wapiganaji wa kundi la al-Qaeda wamevamia na kushambulia uwanja wa ndege wa Sayoun ulioko katika mkoa wa Hadhramaut, kusini mwa nchi hiyo.
Habari zaidi zinasema wanamgambo wa kundi hilo waliuvamia uwanja huo kutoka maeneo matatu na kisha kuuripua mnara wa mawasiliano kwenye angatua hiyo. 

Taarifa za hivi punde zinasema kuwa, maafisa wa serikali wamefanikiwa kuudhibiti tena uwanja huo wa ndege.
 
Huku hayo yakijiri, mripuaji wa kujitolea muhanga amewaua wanajeshi 6 wa Yemen baada ya kugongesha gari lililokuwa na mada za miripuko kwenye kambi moja ya kijeshi mkoani Hadhramaut. 

Raia 3 pia wameuawa kwenye shambulio hilo la kigaidi leo Alkhamisi. Mashambulizi katika mkoa huo yanadaiwa kuwa ya ulipizaji kisasi kutokana na maafisa wa usalama kukamata idadi kubwa ya wanamgambo wa al-Qaeda katika siku za hivi karibuni.

0 comments:

Post a Comment