Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William
Lukuvi, akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuhusu
Maadhimisho ya Siku ya Dawa ya Kulevya Duniani yanayotarajiwa kufanyika
kitaifa jijini Mbeya leo.
Vijana 65 wa Tanzania wamehukumiwa adhabu ya kifo nchini China baada
ya kupatikana na hatia ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Vijana hao ni kati ya zaidi ya 403 wa Tanzania wanaoshikiliwa katika
nchi mbalimbali duniani kwa tuhuma ya kujihusisha na biashara hizo.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi, mjini Dodoma wakati akizungumzia
Maadhimisho ya Siku Dawa za Kulevya Duniani yanayofanyika Juni 26 kila
mwaka.
Lukuvi alisema kuwa kwa mwaka huu maadhimisho hayo ya kesho, kitaifa
yatafanyika katika viwanja vya shule ya msingi Nzovwe jijini Mbeya na
Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
“Tangu mwaka 2008 kumekuwa na wimbi kubwa la vijana wenye asili ya
Kitanzania kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na
nje ya nchi, mpaka hivi sasa idadi yao ni kubwa kiasi cha kufikia zaidi
ya 400, na wanashikiliwa katika nchi mbalimbali ambazo pia adhabu zao
zinatofautiana kulingana na sheria za nchi hizo,” alisema Lukuvi.
NCHI WANAKOSHIKILIWA
Alizitaja baadhi ya nchi ambako vijana hao wanashikiliwa kuwa ni Brazil
(108), Hong Kong (118), Kenya (34), Pakistan (16) na China 65.
Nyingine ni Japan (7), Malawi (5), Uganda (3), Uswisi (2), Marekani (2), Uturuki (1), Botswana (5) na Msumbiji (1).
“Orodha ya nchi waliko vijana hao ni defu zaidi,” alisema.
Akizungumzia maadhimisho hayo kwa nchini, Lukuvi alisema kauli mbiu
yake kwa mwaka huu ni ‘Uteja wa dawa za kulevya unazuilika na kutibika,
chukua hatua’.
AlisemaTanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye tatizo kubwa
la dawa za kulevya kulingana na takwimu za ukamataji wa dawa hizo.
Kwa mujibu wa Lukuvi, kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu kiasi cha
kilo 220 za dawa hizo aina ya Heroine na watuhumwa 18 walikamatwa huku
pia kilo 15.4 za Cocaine zilikamatwa na watuhumiwa saba.
Lukuvi alisema kwa sasa dawa za kulevya ni tishio kubwa kwa maendeleo
ya taifa kwa sababu imethibitika kuwa matumizi yake hupunguza tija na
ufanisi wa nguvu kazi ya taifa.
SHERIA MPYA YAJA
Alisema katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imekamilisha muswada
wa sheria ya dawa za kulevya ambao kama utapitishwa bungeni na kuwa
sheri kama ulivyo, unaweza kusaidia kwa Kiwango kikubwa kupunguza tatizo
hilo.
Lukuvi alisema tofauti na jinsi ilivyo sheria ya sasa, sheria mpya
itaondoa adhabu ya faini na watuhumiwa kunyimwa dhamana wanapokamatwa,
hali ambayo itasaidia kukabiliana na wasafirishaji na wauzaji wa dawa
hizo.
Kwa mujibu wa Lukuvi, sheria hiyo itakwenda sambamba na uundaji wa
chombo imara cha kushughulikia dawa za kulevya ambacho kitakuwa na uwezo
wa kupeleleza, kukamata na kushitaki watuhumiwa wa dawa za kulevya
kama ilivyo kwa Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Alisema kuwa muswada huo tayari umekamilika na kwamba wakati wowote
unaweza kuwasilishwa bungeni ili upitishwe hatimaye kuwa sheria.
Alisema maadhimisho hayo pia yatafanyika katika ngazi ya mkoa nchini
na kuwaomba wananchi kujitokeza kushiriki ili waweze kupata elimu ya
kutosha juu ya madhara na vita dhidi ya dawa hizo.
Jun 26, 2014
Watanzania 65 wauza `unga` kunyongwa China
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment