Dec 1, 2013

Wafungwa 40 wakimbia jela huko nchini Libya

Duru za usalama nchini Libya zinaripoti kuwa, kwa akali watu 40 wametoroka katika moja ya jela za kusini mwa nchi hiyo. 

Duru za usalama mjini Tripoli zimetangaza kuwa, tukio hilo lilitokea kufuatia shambulio la watu wenye silaha lililotekelezwa dhidi ya jela kuu ya mkoa wa Sabha kusini mwa Libya na kupelekea wafungwa 40 kutoroka. 

Mkuu wa jela hiyo Shaban Nasri amesema kuwa, baada ya watu wenye silaha kuvamia jela hiyo walifyatua risasi kwa wingi na kuingia katika seli za wafungwa. 

Ameongeza kuwa, watu hao walikuwa wanalengo la kumtorosha mmoja wa wafungwa aliyekuwa anashikiliwa katika jela hiyo ambapo baada ya kumkosa walianza kuwatishia wafungwa wengine kwa silaha ili wataje mahala alipo mtu wao, suala lililopelekea wafungwa wengine 40 kutoroka jela. 

 Kufuatia tukio hilo, mkuu wa jela hiyo ameitaka Wizara ya Sheria nchini Libya kutoa msaada wa kimada na vikosi vya ulinzi kwa lengo la kuimarisha usalama na ulinzi katika jela kuu ya Sabha nchini humo.

0 comments:

Post a Comment