MASHAMBULIZI
ya wabunge dhidi ya mawaziri wanne kushindwa kusimamia wizara zao,
yamemfanya Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wao kuanzia jana.
Mawaziri hao ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis
Kagasheki, Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Mathayo David
Mathayo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai
Nahodha, na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Awali kabla ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda hajalieleza Bunge, uamuzi
huo wa Rais Jakaya Kikwete, Waziri Kagasheki alitangaza kujiuzulu
wadhifa wake baada ya kuguswa na ripoti ya Kamati Ndogo ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyokuwa ikichunguza madhila yaliyotokana
na Operesheni Tokomeza Ujangili.
Balozi Kagasheki, ameamua kujiuzulu wadhifa wake baada ya kutuhumiwa
kushindwa kusimamia kikamilifu Operesheni Tokomeza Ujangili iliyokuwa
ikifanywa na wizara yake.
Alisema amesikiliza kwa makini sana ripoti ya kamati hiyo na kuamua
kuachia wadhifa huo kutokana na madhila yaliyowapata watu, mifugo na
mali.
“Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete aliponiteua alifanya hivyo kwa furaha
yake na kuamini nitafanya kazi yake vizuri, yametokea yaliyotokea na
yamesemwa mengi… mimi ni mtu mzima nimesoma hisia zenu.
“Nimeamua kujiuzulu wadhifa wangu na nitafuata taratibu zote zinazotakiwa… nitaitaarifu mamlaka ya juu uamuzi wangu,” alisema.
Mara baada ya Kagasheki kutoa taarifa yake hiyo, Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mathayo David Mathayo, alipopata fursa ya kuzungumza, alisema
anaona anaonewa kuhusishwa na ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na
askari waliokuwa kwenye operesheni hiyo.
Aliongeza kuwa kutajwa kwake katika ripoti hiyo kunaonyesha watu walikuwa wana dhamira mbaya dhidi yake.
“Jana usiku nilisoma sana Biblia ambayo ni Zaburi ya 72… nilisali
sana jana usiku kwa kuwa niliona dalili za kuonewa, nawaambia matatizo
mengi yaliyozunguzwa hayakuwa chini ya wizara yangu.
“Kuna wabunge wamesema wazi wazi hapa kuwa ninaonewa kuingizwa katika
mkumbo wa mawaziri wanaotakiwa wawajibike, naapa mbele ya mwenyezi
Mungu Subhana wa taala atawalipa wale walioona ninaonewa kwani nilijua
hili,” alisema.
Mara baada ya Mathayo kuzungumza, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alipewa
fursa ya kuzungumza ambapo alisema amezungumza na Rais Kikwete ambaye
yupo nchini Marekani juu ya jambo hilo na aliungana na wabunge waliokuwa
wakitaka mawaziri hao wawajibike.
Alibainisha kuwa Rais Kikwete pia alitaka kuundwa kwa tume ya
kuchunguza madhila yote yaliyotajwa kwenye ripoti ya kamati ndogo ya
Bunge iliyoundwa kuchunguza sakata hilo.
“Nilipomueleza mambo hayo akasema ametengua uteuzi wake kwa mawaziri
wote wanne, atakuja kuangalia hapo baadae kwa picha iliyojitokeza. Rais
kaona uzito wa tukio hilo, hivyo kaamua kutengua uteuzi wao.
“Tumekubaliana na Rais Kikwete ambaye sasa yupo safarini, akirudi
tutakuja kumalizia mambo yaliyobakia… mawaziri hawa wamejiuzulu si
kwamba walikuwapo kwenye meneo ya tukio au walishiriki bali vyombo
vilivyofanya hivyo vipo chini yao,” alisema.
Pinda alisema pia alizungumza na mawaziri hao juu ya tuhuma
zilizoelekezwa kwao na wabunge pamoja na kamati iliyoundwa na kuchunguza
sakata hilo.
“Nilizungumza nao kwa jambo hilo, niliwaambia wabunge wamesema sana,
niliwambia kwa kuwa wao ni watu wazima wapime mambo hayo, waheshimiwa
hawa wote wamekubali kujiuzulu, wamekubali kujiuzulu kwa sababu mambo
hayo yamefanyika chini ya utawala wao,” alisema.
Mara baada ya Pinda kuzungumza, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji
Fredrick Werema, alisema hatua ya kujiuzulu na ripoti hiyo inafungua
milango ya sheria kuchukua mkondo wake kwa wale wote waliohusika.
“Pia tunaomba Bunge liridhie uundaji wa tume ya uchunguzi wa
kimahakama ambayo tuna hakika itayaangalia mambo yote yaliyotokea kwa
kina zaidi,” alisema.
Dec 21, 2013
Mawaziri wango'oka
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment