Dec 3, 2013

KESI YA PONDA NGOMA MZITO


Maombi ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda ya kuomba ufutiwa shtaka la kukiuka uamuzi wa mahakama, yamebaki njiapanda baada ya Jamhuri kuyawekea pingamizi la kisheria, ikiiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iyatupilie mbali.
 

Sheikh Ponda, kupitia kwa Wakili wake Juma Nassoro, aliwasilisha mahakamani hapo maombi ya marejeo, akiiomba mahakama hiyo ifanye marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.

Maombi hayo yalitarajiwa kuanza kusikilizwa jana lakini, Serikali iliwasilisha pingamizi hilo la awali na hivyo mahakama hiyo ikalazimika kuanza kusikiliza pingamizi hilo kabla ya kuendelea na maombi ya msingi. Pingamizi hili liliwasilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu (PSA), Bernard Kongola.

Wakili alidai kuwa hati ya kiapo inayounga mkono maombi hayo ni batili kwa kuwa ina kasoro za kisheria.

Alibainisha kasoro hiyo kuwa ni kutokuwa na tarehe ambayo kiapo hicho kilitolewa na kwamba hakuna mahali panapoonyesha kuwa msimamizi wa kiapo alikuwa akimjua mla kiapo na wala kueleza kuwa mla kiapo alitambulishwa kwake na nani.

Wakili Kongola alieleza kuwa hata kwenye hati ya kiapo iliyoko katika jalada lililoko mahakamani inaonyesha kuwa kuna kasoro hizo na kwamba walijiridhisha hivyo baaada ya kudurusu katika jalada hilo la mahakamani.

“Mheshimiwa Jaji, dosari hizi haziwezi kurekebishika, kwa hiyo maombi yote ni batili,” alisema Wakili Kongola.

Hata hivyo, Wakili wa Ponda, Nassoro alisema kiapo hicho ni sahihi na kimetimiza matakwa ya kisheria kwa kuwa nakala aliyonayo inaonyesha kiapo hicho kilitolewa na Oktoba 8, 2013 na kwamba, msimamizi wa kiapo alikuwa akimfahamu mla kiapo, ambaye ni Ubaidi Hamidu.

Pia wakili Nassoro alisema Serikali haijatoa ushahidi mahakamni kuonyesha kuwa kweli ilidurusu jalada la mahakama na kubaini kuwa hati hiyo iliyoko mahakamani ina dosari hizo wala kueleza ni lini alifanya hivyo hivyo.

Akijibu hoja hiyo Wakili Kongola alisisitiza kuwa kiapo hicho ni batili kama walivyojiridhisha kwenye jalada la mahakama, Novemba 21, 2013, na kwamba wanao ushahidi wa kutosha katika hilo. Baada ya kusikiliza hoja hizo, Jaji Rose Teemba anayesikiliza maombi hayo aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 11.

0 comments:

Post a Comment