Nov 2, 2013

Viongozi Kuhukumiwa na Wanachama

CHAMA cha Wananachi (CUF), kimesema hatma ya Katibu Mkuu wao, Maalim Seif Sharif Hamad kuendelea na uongozi, ipo mikononi mwa wapiga kura wa chama hicho kwa kuwa katiba inamruhusu kuwania nafasi hiyo atakavyo.

Mbali na Seif, pia chama kimesema kiongozi yeyote aliye madarakani kwa sasa ana uhuru wa kutetea nafasi yake ilimradi akidhi vigezo vya kupitishwa kuwania nafasi atakayoomba.

Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Naibu Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Bunge wa CUF, Shaweji Mketo, alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea mchakato wa uchaguzi ndani ya chama unaotarajiwa kumalizika Mei mwakani.

Mketo alisema kuanzia jana wameshaanza taratibu za uchaguzi ndani ya chama baada ya makubaliano na kamati ya utendaji iliyokaa hivi karibuni kuangalia umuhimu wa uchaguzi huo katika kuelekea chaguzi mbalimbali za kitaifa.

“Tunafanya uchaguzi kujiandaa na uchaguzi mbalimbali wa kitaifa kuanzia ule wa serikali za mitaa mwakani na ule wa rais na wabunge 2015, tumedhamiria kuongoza nchi kwa kupanga safu imara ya uongozi,” alisema.

Alisema uchaguzi kwa ngazi ya matawi ulioanza jana, utamalizika Novemba 30 mwaka huu, ngazi ya kata utaanza Desemba Mosi na viongozi wa ngazi hiyo watakuwa wamepatikana ifikapo Januari 10 mwakani.

Mketo aliongeza kuwa ngazi ya wilaya uchaguzi utaanza Januari 11 hadi 18 mwakani na viongozi watakuwa wamepatikana ifikapo Machi 20, huku ngazi ya taifa ukianza Machi 28 kwa wagombea kuchukua fomu na kurudisha, na uchaguzi utakuwa umekamilika ifikapo Mei 31, 2014.

0 comments:

Post a Comment