Nov 15, 2013

UISLAMU Si Dini Ya Mabomu

SHEIKH wa Jumuia ya Wahamadiyya Tanzania, Tahir Chaudhry amesema Uislamu si dini ya ugomvi au kuvaa mabomu kama baadhi ya watu wanavyoamini.

Pia ameitaka jamii kuacha kutumiwa vibaya na baadhi ya makundi yanayojihusisha na vitendo vya ugaidi kupitia mgongo wa dini.   

Alitoa mwito huo juzi wakati akihutubia kongamano la amani lililoandaliwa na Jumuia ya Waislamu wa Ahmadiyya Mkoa wa Ruvuma ambalo lilijumuisha viongozi mbalimbali wa dini, wanasiasa na wananchi.   

Chaudhry alisema baadhi ya watu wamekuwa wakitumiwa vibaya katika kufanya vitendo vya kuleta machafuko katika nchi kwa kuwaua binadamu wenzao, kujilipua na kujitoa mhanga kwa kupitia mwamvuli wa dini jambo ambalo ni kinyume cha maagizo ya Mwenyezi Mungu.

Alisema lengo la kufanya kongamano hilo ni kutoa ufafanuzi kuhusu Uislamu kuwa ni upendo daima na si kugombana kwani kumekuwepo na tafsiri potofu kwamba Uislam ni dini ya ugomvi jambo si sahihi.

“Uislamu si kuvaa mabomu na kujilipua ili kudhuru wengine bali ni kujenga upendo na amani mbele za jamii kwa kuwa hakuna mtu atakayefika kwa Mungu kwa kujilipua mabomu,” alisema.   

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu aliipongeza jumuia hiyo kwa kuandaa kongamano la kuzungumzia amani na kubainisha kuwa hilo ni jambo jema.   

 Alisema amani inapotoweka hakuna mbadala wake na Tanzania ndiyo nchi pekee ya kutiliwa mfano kwa kuwa imekuwa kimbilio la nchi ambazo zimefarakana na kupongeza viongozi wa dini kuhubiri amani.   

Sheikh wa Kanda Mbeya, Bashart-U-r-Rehman alisema lengo la Waislamu wa Jumuia ya Wahamadiyya Tanzania ni kufanya kongamano nchi nzima na endapo litafanikiwa linaleta mafanikio makubwa kwa jamii.

Kwa upande wake, Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Songea, Nicodem Mbano alisema ili amani iendelee kudumu ni lazima viongozi wake watende haki kwa wananchi wanaowaongoza.

Mbano alisema suala la haki na amani ni vizuri likaingizwa kwenye mtaala ili liweze kufundishwa shuleni kuanzia msingi hadi vyuo vikuu kwa lengo la kuwajengea uwezo vijana kulielewa kwa kina.

0 comments:

Post a Comment