MWANAFUNZI wa Chuo cha Slafia Bunju A, Dar es Salaam, Nasibu
Chipoto (23), ameumia vibaya baada ya kudai kufanyiwa unyama na jirani
ambaye ni raia wa Kongo.
Makamu Mkuu wa chuo hicho cha
Kiislam, Abdallah Yusuf, alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 28 mwaka
huu, saa 3: usiku.
Yusuf alisema wanafunzi wa chuo hicho wana kawaida ya kuchota maji
katika nyumba hiyo, hivyo siku ya tukio Chipoto alikwenda kuchota maji
ndipo alipovamiwa na mmiliki wa nyumba hiyo na kumfunga kamba mikono na
miguu na kuanza kumpa mateso.
Alidai mmiliki huyo kwa kushirikiana na mkewe na wafanyakazi wake
watatu walimpiga kijana huyo huku wakimchoma na pasi ya umeme mwilini
na kumsababishia maumivu makali.
Makamu huyo alidai baada ya kusikia kelele walikwenda eneo hilo, ili
kumuokoa kijana huyo lakini mmiliki huyo alitoa bastola na kuwatishia
ndipo wakaamua kukimbilia kituo cha polisi kutoa taarifa.
“Kijana wetu alipata mateso makali; wale watu walimfunga mikono
wakampiga huku yule mmiliki akimchoma na pasi mwili mzima. Mbaya zaidi
akatutishia kwa kutufyatulia risasi tulipotaka kumuokoa,” alieleza.
Alidai wakiwa kituo kidogo cha polisi cha Wazo kabla hawajaondoka,
mmiliki huyo alifika akiwa amembeba kijana huyo huku akidai kuwa ni
mwizi.
Yusuf alidai kuwa kutokana na hali ya kijana huyo kuwa mbaya polisi
walimweka chini ya ulinzi mmiliki huyo na kijana huyo kupewa PF3 na
kwenda kutibiwa hospitali ya Mwananyamala.
“Tunamshukuru Mungu sasa Chipoto anaendelea vizuri na yuko kwa ndugu
zake Mbagala ila huyu mtuhumiwa tunasikia ameachiwa kwa dhamana,”
alidai.
Alipoulizwa Kamanda Wambura alisema hana taarifa juu ya tukio hilo na kuahidi kulifuatilia na kutoa taarifa.
|
0 comments:
Post a Comment