Nov 9, 2013

Afia ndani ya Gari Akiwa na Madawa Ya Kulevya

MAITI ya kijana Kassim Said Mboya (36), mkazi wa jijini Dar es Salaam, imekutwa na kete 65 zinazodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya.

Maiti ya kijana huyo, ilikutwa katika basi la Kampuni ya Taqwa eneo la Kasulumu lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea nchini Malawi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kumtaka mwandishi akutane naye eneo la chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa ajili ya kuona mwili wa marehemu huyo.

Alisema kijana huyo kabla ya kifo, alikamatwa Novemba 7, mwaka huu, akiwa ndani ya basi hilo lenye namba za usajili T 319 BLZ akiwa na tiketi yenye jina la Kassim Mueck Michael.

“Awali basi hilo kabla ya kufika mpakani Kasumulu na abiria kushuka na kuanza kufanya taratibu za kuvuka kuingia nchini Malawi, kijana huyo alibaki kwenye gari huku afya yake ikizidi kudhoofika,’’ alisema.

Alisema baada ya kuona hivyo, wahusika wa basi hilo walitoa taarifa kituo cha polisi ambapo kijana huyo alichukuliwa na kupelekwa katika hospitali ya Wilaya ya Kyela na kabla hajapata matibabu alifariki dunia.

Kwamba, kijana huyo alikuwa na dalili zilizogundulika kuwa alikuwa na dawa za kulevya, ndipo iliamriwa mwili wake kusafirishwa hadi hospitali ya Rufaa ya Mbeya ambako ulipasuliwa na kukutwa na pipi 65 zinazodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya na moja ikiwa imepasuka.

“Natoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Mbeya na nchi nzima kwa ujumla kufika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa ajili ya utambuzi wa mwili wa marehemu,’’ alisema.

Hii ni maiti ya tatu kukutwa na dawa zinazodhaniwa kuwa za kulevya mkoani Mbeya, ambapo shehena ya kwanza ya dawa hizo ilikamatwa mwaka jana mjini Tunduma mkoani hapa mwaka 2006, ikiwa kwenye tumbo la marehemu Kombo Siriri.

Shehena ya pili ya dawa hizo ilikamatwa Desemba 5, 2011, katika hotel ya High Class mjini Tunduma, ikiwa katika tumbo la maiti ya Mshanga Mwasala.

Licha ya ukamataji wa dawa hizo na baadhi ya watuhumiwa wakiwa hai, hakuna mtuhumiwa aliyewahi kupatikana na hatia tangu mfululizo wa ukamataji dawa hizo mkoani Mbeya.

0 comments:

Post a Comment