MTOTO wa miezi 10, aliyetambuliwa kwa jina la Fahazal mkazi wa
Kivunge amefikishwa mbele ya serikali ya mkoa wa kaskazini Unguja, baada
ya mama yake mzazi kusema amekuwa akitokewa na maajabu na kwamba jamii
iombe dua ili kunusuru kutokea vifo.
Mtoto huyo, ambaye anaishi katika kijiji cha Changani Kivunge wilaya
ya Kaskazini ‘A’ Unguja, ameonesha maajabu, baada ya kuanza kusema akiwa
na umri wa miezi miwili, kwa kutaja majina ya Mwenyezi Mungu, Mtume
Muhammad (SAW) na maneno ya kumtukuza Mwenyezi Mungu.
Mkuu wa wilaya hiyo, Riziki Juma Simai, akizungumza na Zanzibar Leo, amethibitisha kuwepo mtoto huyo.
Alisema mtoto huyo amefikishwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa na familia yake
baada ya mama yake aliyefahamika kwa jina moja la Dawa, kutakiwa
kuwasilisha ujumbe alionao mtoto huyo kwa jamii.
Alisema kabla ya kuzaliwa, mama yake alisema kuwa alikutwa na mambo
ya maajabu baada ya kujiwa na kiumbe akimueleza uwezo wa mtoto wake
wakati akiwa tumboni na kumchagulia jina la kumpa baada ya kuzaliwa.
Mkuu wa wilaya huyo alisema, kiumbe hicho kilichokuwa katika
mazingira yasioelezeka pia kilimtabiria mama huyo kwamba atazaa mtoto wa
kiume.
Pia alimuambia baada ya mtoto huyo kuzaliwa atakuwa na mambo ya ajabu
na kumtaka kumtunza na asimuogope na baadae kiumbe hicho kiliondoka.
Alisema baada ya tukio hilo, na siku zake za kuzaa kutimia
alijifungua mtoto wa kiume na kumpa jina la Fahazal na ndipo alipoanza
kushuhudua maajabu ikiwa ni pamoja na kuzungumza akiwa na miezi miwili.
Alisema mtoto huyo alikuwa akitamka maneno ya kumtukuza Mwenyezi
Mungu ikiwemo Allwah, Yaraabi na kutaja jina la Mtume (SAW) huku
akiwataja kwa majina watu waliokuwemo nyumbani kwao.
Mkuu wa wilaya hiyo alisema hivi sasa mtoto huyo, amekuwa akiwasomea
dua watu wanaofikishwa kwake kwa matatizo ambapo huonesha ishara ya
kuinua mikono juu ya kuitikia dua wakati ikisomwa.
Alisema kwa muda mrefu, familia yake iliendelea kuishi naye, lakini
mama yake alifuatwa tena na kiumbe hicho na kumtaka kufikisha ujumbe wa
mtoto huyo mbele ya jamii akitaka jamii iombe dua kwa wingi kwani vifo
vingi vinaweza kutokea nchini.
Alisema kiumbe hcho kilirudi baada ya mama wa mtoto huyo kupuuza
ujumbe wa mwanzo aliopewa na ndipo alipoamua kutafuta watu wa kumsaidia
ambapo walimuelekeza kufuata viongozi wa dini.
Alisema, baada mama huyo kupokea ujumbe huo, aliamua kuutekeleza kwa
kuwafuata baadhi ya walimu katika kijiji hicho kuelezea mkasa huo, ili
aweze kupata msaada.
Viongozi wa dini walimtaka mama huyo, kulifikisha suala hilo katika
ngazi ya serikali, kutokana uzito wake kwa jamii, ambapo walimshauri
kuonana na uongozi wa mkoa.
Mkuu huyo wa wilaya alisema, jana asubuhi, alimpokea mama huyo akiwa
na mtoto wake pamoja na shahidi ambaye ni mkaazi wa kijiji hicho ambapo
walithibitisha maajabu ya mtoto huyo.
Alisema mtoto huyo huzungumza baadhi ya wakati na kwamba anazungumza lugha tofauti ikiwemo kiingereza, kiarabu.
Alisema wameifikisha familia hiyo kwa Mkuu wa Mkoa ili kufanyiwa
mahojiano zaidi ambapo serikali itajua nini la kufanya hapo baadae.
Alisema wanalazimika kulifanyia kazi suala hilo, kwa vile tayari
imetolewa tahadhari ya kutokea balaa litakalowahusisha watu wengi.
Munira blog imefanikiwa kupata picha ya video ya mtoto huyo namna anavyolitamka jina la ALLAAH.
Habari hizi ni kwa hisani ya zanzibar leo
0 comments:
Post a Comment