Aug 31, 2013

WENGI WANAFUNGWA PASIPO HATIA


 WAZIRI WA SHERIA NA KATIBA MHE.MATHIAS CHIKAWE

ASILIMIA 70 ya wafungwa nchini wamefungwa kwa kukosa msaada wa sheria, imefahamika. Ongezeko la ada ya kufungulia kesi mahakamani nalo limesababisha kupunguza upatikanaji wa haki kwa kundi kubwa la watu masikini hususan katika kesi za ardhi.

Utafiti uliofanywa na Mtandao wa Shirika Linaotoa Huduma ya Msaada wa Sheria (TANLAP) ya Dar es Salaam, unaonyesha kesi za wafungwa wengi zilikuwa na nafasi ya kuzishinda na kuachiwa huru na Mahakama kama wangeweza kupata wanasheria wa kuwatetea.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANLAP, Christina Kamili alisema ripoti ya utafiti ya 2011/2012 inaonyesha msaada wa sheria unahitajika kwa watu wenye tabaka la chini ambao hawana uwezo wa kuwalipa mawakili.
Alisema kuna vituo vichache vyenye uwezo wa kutoa msaada wa sheria vyenye uwezo wa kustahili kuandika barua ya msamaha wa ada ya mahakama, hivyo kuacha wananchi wengi wanaohitaji msaada huo.

“Tanzania haina sheria ya kuwapo usaidizi zinazotoa mwongozo katika utekelezaji na udhibiti wa utoaji huduma za msaada wa sheria nchini.

“Suala la wananchi kupata haki ya sheria linapaswa kuwa la katiba kwa sababu si wote wanaofungwa gerezani wana makosa. Wengi wao wanashindwa kujieleza ndiyo maana wanafungwa.

Mkurugenzi huyo alisema utafiti huo unaonyesha kuwa ukosefu wa vituo vya sheria na mawakili katika maeneo ya pembezoni hususan vijijini, linasababisha wananchi wengi kukosa haki hiyo.

Naye Ofisa kutoka Wizara ya Sheria na Katiba, John Rwabuhanga, alisema Serikali ipo katika mchakato wa kutengeneza sheria inayohusu misaada ya sheria kwa watu masikini ambao hawana uwezo wa kulipa mawakili katika kesi zao mbalimbali.