"Mbu maarufu zaidi ni jike aina ya Anopheles ambaye huambukiza malaria.
Kwa kawaida, mbu huyu hutegemea mimea kujilisha, lakini anahitaji viini
lishe vilivyomo kwenye damu kwa ajili ya kutaga mayai na kuzaliana."
Mbu ni mdudu msumbufu kwa wengi,
ingawa kuna wengine katika jamii yetu ambao si chaguo lake.Mvua zinanyesha, joto ni kali jijini Dar es Salaam, madimbwi ya maji yamezagaa kila mahali hiyo ikiwa ni ishara kuwa mbu nao wamepata makazi, wamesambaa kila eneo.
Kusambaa kwao ni mwanzo wa madhara kwa jamii kwani ugonjwa wa malaria nao unashika kasi. Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) vifo zaidi ya milioni moja na matukio zaidi ya 400 milioni husababishwa na malaria katika nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara.
Malaria hayo husababishwa na mbu jike aina ya anopheles ambao wana tabia za ajabu, kwani wanachagua nani wa kung’ata na yupi hafai kung’atwa.
Wataalamu wa tabia za mbu wamegundua kuwa mbu huchagua binadamu wa kumuuma kulingana na umbile, harufu na tabia za binadamu huyo.
Kwa nini mbu ni wabaguzi namna hii?
Kitaalamu inaelezwa kuwa kuna makundi zaidi ya 3,500 ya mbu duniani na kati ya hayo mengi yanajilisha yenyewe kupitia mwili wa binadamu.
Mbu maarufu zaidi ni jike aina ya anopheles ambaye huambukiza malaria. Kwa kawaida, mbu huyu hutegemea mimea kujilisha, lakini anahitaji viini lishe vilivyomo kwenye damu kwa ajili ya kutaga mayai na kuzaliana.
Harufu ya mwili na jasho
Dk Fredos Okumu, mwanasayansi na mtafiti wa Kitengo cha Afya ya Mazingira katika Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI) anasema ni kweli kuwa mbu wana tabia ya kuchagua mtu wa kumuuma kwani wana uwezo wa kunusa na kutambua harufu, unyevu na joto la mwili, lakini zaidi hasa harufu kwani kila mmoja ana harufu yake.
Anasema Dk Okumu kuwa mwili wa binadamu huzalisha kemikali tofauti zaidi ya 500 ambazo nyingi kati ya hizo hutambuliwa kwa urahisi na mbu kwa kutumia antenna mbili zilizo vichwani mwao. Tafiti zinaonyesha kuwa mbu wanavutiwa zaidi na harufu za mwili zitokanazo na tindikali aina ya lactic na ile ya uric na harufu ya pombe(ethanol).
Kemikali aina ya lactic hutolewa nje kupitia vitundu vidogo katika ngozi na huzalishwa baada ya mazoezi.