Mar 21, 2016

Pemba wazira, Unguja wachechemea

mtanzaniadaily .indd
HATUA ya kupiga kura kisiwani Pemba jana ilifanyika kwa utulivu huku kukiwa na idadi ndogo ya wapiga kura wakati kwa upande wa Unguja watu walijitokeza ingawa  kwa idadi ambayo si ya kuridhisha.

Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Chama cha Wananchi (CUF) kutangaza  kususia uchaguzi huo wa marudio.

Uchaguzi huo wa marudio ulifanyika baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha,   kufuta uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 akidai kuwa ulikiuka sheria na taratibu.

CUF kilipinga kufutwa kwa uchaguzi huo kikidai kuwa kilikuwa kimeshinda na kikatangaza kutoshiriki marudio yake.

Kisiwa cha Pemba chenye majimbo 18 ya Uchaguzi ni ngome ya CUF na katika uchaguzi huo kilishinda  majimbo yote kwa nafasi za Ubunge na Wawakilishi.

Kutokana na kujitoa kwa CUF katika uchaguzi wa marudio, jana vituo vingi vya kupiga kura vilivyofunguliwa tangu saa 1.00 asubuhi, vilikuwa na watu wachache na ilipofika saa 5.00   vingi vilikuwa wazi huku baadhi ya wasimamizi wakijilaza kwenye madawati na meza.

Akizungumzia hali hiyo, mmoja wa wasimamizi katika kituo cha Wawi ‘A’, Ismail Issa, alisema kujitoa kwa CUF kumesababisha wananchi wengi wasipige kura.

“Watu ni wachache sana ikilinganishwa na uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 ambako kulikuwa na misururu ya watu wengi hadi saa 10.00 alasiri. Leo hadi saa 3.00 hii hakuna watu,” alisema Issa.

Alisema kituo hicho chenye wapiga kura 1400 kilitarajia kupata asilimia 20 ya wapiga kura.

Akizungumzia hali hiyo, Mgombea urais wa Chama cha ADC, Hamad Rashid, alisema kisiwa hicho ni ngome ya CUF ingawa akisema kujitoa kwao hakutaathiri utendaji wa Serikali.

“Hii ni ngome ya CUF, kisiwa hiki kina majimbo 18 na yote waliyachukua, lazima tukubali hilo, ndiyo maana waliojitokeza leo ni wachache. Lakini hakuna athari yoyote ya kujitoa kwao.

“Mwaka 2003 tulipiga kura ya maruhani, walioshinda walipata mamia ya kura na walioshindwa wakiwa na maelfu, lakini Serikali iliendelea,” alisema Rashid.

Rashid alisema ameamua kushiriki uchaguzi huo kwa kuwa ni haki yake na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi na wasiotaka wasiwabugudhi wengine.

“Tunataka kupata Serikali, tunataka kuingia kwenye maendeleo. Tatizo letu kubwa ni ajira kwa vijana wanaokaa vijiweni.

“Ndiyo maana namuunga mkono Rais John Magufuli kwa kauli yake ya Hapa Kazi tu na sisi ADC tunasema Hapa ni Wajibu Tu,” alisema Hamad,

Hamad Rashid,  anatajwa kuwa huenda ndiye akawa makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.

Mgombea urais huyo wa ADC,  alisema kwamba hakuna chama kidogo kwenye siasa na lolote linaweza kutokea.

“Hakuna chama kidogo. Mwaka 1963 kulikuwa na vyama vya ASP na ZNP vilivyopata viti 10 kila kimoja huku chama cha ZPPP kikipata viti vitatu.

“ ZPPP kiliungana na ZNP na kiongozi wake ndiye akawa Waziri Mkuu. Kwa hiyo mambo hubadilika, unaweza kusikia Hamad akawa Rais,” alisema.

Ingawa alikiri kuwapo   matatizo katika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), aliendelea kutetea chama chake kushiriki uchaguzi huo akisema ndiyo njia bora ya kurekebisha kasoro.

“Hivi ukiumwa na mkono ndiyo uukate?  Hapana utautibu. Mbona hao wanaoikosoa ZEC hawatoki? Ni wanachama wa CUF lakini hawatoki. Huwezi kuirekebisha ZEC bila kuwa na Baraza la Wawakilishi,” alisema.

Mbali na Hamad Rashid, mgombea urais mwingine aliyefika kupiga kura kwenye kituo hicho alikuwa Mwenyekiti wa AFP, Said Soud Said aliyejipa matumaini ya kushinda.

“Nashukuru tumepiga kura na Mungu ameleta manyunyu, hii ni ishara ya neema. Hata siku ya kiama kutakuwa na manyunyu. Watu wamepiga kura na watapata kiongozi mpya ambaye ni mimi.

“Kujitoa kwa CUF hakutaathiri chochote kwa sababu hata mwaka 2003 walipiga kura za maruhani lakini Serikali ikaendelea tu,” alisema Said.

Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Zanzibar, Mohamed Aboud, aliyekuwa akizunguka katika vituo mbalimbali vya kupigia kura, alikiri kuwapo   idadi ndogo ya wapiga kura lakini akasema wanatarajia kupata angalau asilimia 40.

‘Nawashukuru wananchi kwa kujitokeza kupiga kura, natoa wito waendelee kupiga kura.

 Ni kweli kuna uchache wa watu, lakini hauleti mshtuko kwa sababu kila upande una wanachama wake.

“Hapa Pemba kuna wanachama wengi wa CUF na kule Unguja kuna wanachama wengi wa CCM. Tunatarajia kupata angalau asilimia 40 ya wapiga kura,” alisema Waziri Aboud.

Katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, hali ya usalama ilikuwa shwari   huku idadi ya watu waliojitokeza ikiwa ndogo zaidi.

Wasimamizi wapiga usingizi
Baadhi ya wasimamizi katika kituo cha Shule za Kizimbani na Kunjwi walionekana kulala kwenye meza kwa kukosa wapiga kura huku polisi wakijipumzisha kwenye viti.

Mkuu wa Wilaya ya Wete, Rashid Khalid Rashid,    alisema hali ya usalama imeimarishwa na wapiga kura wamejitokeza.

“Hali ya usalama iko shwari   na vijana tuliowatarajia wamekuja kupiga kura. Hata hivyo, ikilinganishwa na uchaguzi wa Oktoba 25, waliopiga kura sasa siyo wengi,” aliema Rashid.

Katika vituo mbalimbali, CCM iliweka mawakala watatu wanaowakilisha Rais, Mbunge na Diwani, huku vyama vingine vya ADC na Tadea vikiwa na wakala mmoja mmoja.

Usalama
Hali ya usalama ilikuwa imeimarishwa katika maeneo mengi huku magari yaliyosheheni polisi na magari ya Jeshi la Wananchi  wa Tanzania (JWTZ) yakiranda mitaani.

Vilevile,  mitaa mingi haikuwa na watu na maduka na hoteli nyingi zilikuwa  zimefungwa.
Mwisho

0 comments:

Post a Comment