Mar 21, 2016

MWANDISHI ALIYETEKWA AKUTWA HOSPITAL


Mwandishi wa gazeti la Mwananchi na DW, Salma Said.

Dar es Salaam.
Siku tatu baada ya mwandishi wa Mwananchi na DW, Salma Said kutoweka, jana alipatikana baada ya kukutwa katika Hospitali ya Regency ya jijini hapa na kupelekwa kituo kikuu cha polisi kuhojiwa.

Habari zilizopatikana jana jioni na kuthibitishwa na mumewe, Ali Salim Khamis na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi, Simon Siro zilisema Salma alisajiliwa jana mchana katika hospitali hiyo.

Ali aliyekuwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, alisema kwa ufupi kuwa amepata taarifa hizo na kufika Dar es Salaam kuzifuatilia.

Kamanda Siro alisema ni kweli Salma amepatikana na ametumwa mkuu wa upelelezi wa kanda hiyo kumfuata hospitali ampeleke kituoni kwa mahojiano. Mpaka tunakwenda mitamboni Salma alikuwa anahojiwa.

Awali, wadau wa habari waliungana na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), kueleza hofu yao kutokana na kutoweka kwa mwandishi wa habari, Salma Said na kuvitaka vyombo vya dola kulitafutia ufumbuzi wa haraka suala hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na MwanaSpoti, Francis Nanai alisema wanaendelea kufuatilia kwa makini suala hilo.

“Taarifa za kutoweka kwa Salma zilitufikia Ijumaa mchana Machi 18, 2016 kupitia kwa mume wake, mpaka sasa hakuna taarifa yoyote inayoonyesha ni nani au chombo gani kinamshikilia au kumhifadhi, hali hii inatutia wasiwasi mkubwa kama kampuni na wadau wa habari nchini,” alisema Nanai.

0 comments:

Post a Comment