Mar 19, 2016

MWANDISHI AKAMATWA


Mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Salma Said

Dar.
Mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Salma Said jana alikamatwa na watu wasiojulikana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume mjini Unguja, alipokuwa akisafiri kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kuangalia afya yake. 


Akizungumza na mwandishi wetu, mume wa Salma, Ali Salim Khamis ambaye pia ni Mbunge wa Mwanakwerekwe (CUF), alisema alipata ujumbe wa maandishi kutoka kwa mkewe kwamba amekamatwa.

Khamis alisema alipokwenda uwanja wa ndege aliambiwa na mkuu wa polisi wa uwanjani hapo kwamba hana taarifa za tukio hilo jibu ambalo alilipata pia kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mjini Magharibi.

Alisema aliamua kwenda kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa ambako pia aliambiwa hawana taarifa za kukamatwa kwa Salma.


“Hadi sasa sijui mke wangu yuko wapi bado naendelea kumtafuta.”

Khamis alisema Salma alikuwa tayari amepitia taratibu zote na alikuwa akisubiri kuingia ndani ya ndege ambayo haikutajwa, lakini alisema ndege hiyo iliyokuwa iondoke saa 8.05 mchana alizuiwa na watu hao wanaodaiwa kuwa ni askari hadi saa tisa kasoro na walipoiruhusu lakini ikidaiwa kuwa waliondoka na Salma kwenda kusikojulikana.

0 comments:

Post a Comment