Mar 19, 2016

Israeli yazidi kuhujumu vyombo vya habari Palestina


Israeli yazidi kuhujumu vyombo vya habari Palestina
Shirika moja la kutetea uhuru wa kujieleza na haki za waandishi wa habari limefichua kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha hujuma zake dhidi ya taasisi hiyo muhimu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Ripoti ya kila mwaka ya shirika la Palestinian Center for Development and Media Freedoms (MADA) imeonyesha kuwa visa karibia 600 vya kuhujumiwa waandishi wa habari au chombo cha habari vilifanywa na utawala haramu wa Israel mwaka jana pekee wa 2015. 

Moussa Rimawi, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo amesema visa hivyo vya mwaka jana vimevunja rekodi ikilinganishwa na ripoti zake za miaka ya nyuma. 

Rimawi amesema ukiukwaji wa haki za waandishi wa habari katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza umeongezeka kwa asilimia 29 tangu mwaka 2014. 

Ripoti hiyo ya shirika la kutetea uhuru wa vyombo vya habari na haki za waandishi wa habari huko Palestina la MADA imebainisha kuwa, jeshi la utawala huo katili ndilo limehusika pakubwa kwenye hujuma hizo, yaani kwenye takriban asilimia 70 vya visa hivyo; huku kesi 112 zikiripotiwa mwezi Oktoba pekee mwaka jana. 

Mbali na kuua waandishi wa habari kama vile Ahmed Jehajehah katika kambi ya wakimbizi ya Qalandiya na mpiga picha wa Kipalestina Kamal Abu Nahel, maafisa usalama wa utawala huo ghasibu walivamia na kufunga vituo 3 ya redio katika Ukingo wa Magharibi kati ya Oktoba na Novemba, sambamba na kushambulia na kufunga ofisi za kanali za televisheni za Palestine Today na TransMedia.

0 comments:

Post a Comment