Mar 5, 2015

MAKALA;Kupaa, kutunguliwa na kupaa kwa Seif Shariff Hamad Zanzibar








huyu ndie Maalim Seif


Joseph Mihangwa Toleo la 3954 Mar 2015




JANUARI 1984, Halmashauri Kuu [NEC] ya Chama Cha Mapinduzi [CCM]
iliyoketi kwa dharura mjini Dodoma, ilimvua Rais wa Awamu ya Pili wa
Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, nyadhifa zote za chama na serikali,
Visiwani na kwenye Serikali ya Muungano kwa “dhambi” ya kuhoji muundo
upi wa Muungano uliokusudiwa; na kwa kuandaa hati ya mashitaka kutaka
Mahakama Maalum ya Katiba itoe tafsiri na uamuzi juu ya utata huo.





Kutekeleza hilo, Jumbe alitumia ibara ya 125 na 126 ya Katiba ya
Muungano ya mwaka 1977, ambazo zinaipa uwezo na mamlaka Mahakama hiyo
“kusikiliza shauri lililotolewa mbele yake na kutoa uamuzi wa usuluhishi
juu ya jambo lolote, iwapo tafsiri hiyo au utekelezaji wake
unabishaniwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar”.



Nyadhifa alizovuliwa kwa kujaribu kukanyaga “patakatifu” hapo bila
kuvua viatu, ni pamoja na Urais na Uenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Zanzibar, Umakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano; Umakamu Mwenyekiti wa
CCM na Ujumbe wa NEC na Kamati Kuu ya CCM.



Sababu za kuitishwa kikao hicho cha dharura, ilikuwa ni kufuatia
kuibwa kwa Hati hiyo ya Mashitaka iliyoandaliwa kwa niaba ya Jumbe, na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Zanzibar wa wakati huo, Abubakar Swanzy
na kufikishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwalimu Julius Nyerere
kabla Jumbe hajaitia sahihi, ambapo inanong’onwa kwamba Seif Shariff
Hamad, alikuwa mmoja wa waliofanikisha kuibwa kwa Hati hiyo na kumfikia
Mwalimu. Hamad aliwahi kuwa mwanafunzi wa Jumbe wakati akisoma elimu ya
sekondari katika skuli ya Lumumba.



Kufuatia kutunguliwa kwa Aboud Jumbe, Ali Hassan Mwinyi aliteuliwa
Rais wa awamu ya tatu Zanzibar, kuchukua nafasi ya Jumbe; na Seif
Shariff Hamad akapaa kwa kuteuliwa kuwa Waziri Kiongozi kuchukua nafasi
ya Brigedia Ramadhan Haji, aliyetunguliwa pamoja na Jumbe.



Uongozi Visiwani chini ya Mwinyi na Hamad ulikonga roho za wengi,
Bara na Visiwani, kwa sera zake za uwazi na katika nyanja za kufufua
uchumi na kuanzisha sera na soko huria, zilizomkera Mwalimu Nyerere kwa
hofu ya kuuwa “ujamaa”.



Hata hivyo, furaha hiyo haikudumu baada ya Mwinyi kuteuliwa kugombea
nafasi ya Rais wa Muungano miezi 18 baadaye, kufuatia kustaafu
[kung’atuka] kwa Rais Nyerere.



Kutunguliwa kwa Jumbe na Ramadhan Haji kulizua taharuki, kutoelewana
na kuzua makundi miongoni mwa Uongozi wa Zanzibar, huku kundi moja,
lililojiita “Liberators” [Wakombozi] na wahafidhina wa sera za hayati
Karume wakijiona pia kama wamiliki wa Zanzibar, likiona Jumbe kaonewa;
na kundi la pili la “wenye maono” ya Zanzibar mpya, lililojiita
“Frontliners” [Wanamstari wa mbele], akiwamo Seif Shariff Hamad, likiona
hatua iliyochukuliwa na NEC ilikuwa sahihi katika kuimarisha Muungano.



Kufuatia kupendekezwa kwa Mwinyi kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano, nafasi ya Rais Visiwani ilibaki wazi; na katika kikao cha
uteuzi, “Wakombozi” walitaja kwa kelele na nderemo jina la aliyekuwa
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Abdul Wakil Nombe; ambapo
wanamstari wa mbele walimtaja Hamad kwenye kikao cha Kamati Kuu [CC] cha
uteuzi na majina kupelekwa NEC kupigiwa kura, ambapo Wakil alimshinda
Hamad kwa tofauti ndogo ya kura saba tu kati ya wajumbe 1,746 wa NEC
waliopiga kura siku hiyo, Agosti 15, 1985.



Hata hivyo, taarifa za Ki-intelijensia zilitoa nafasi ndogo kwa Wakil
kuweza kupata asilimia 50 ya kura katika Uchaguzi Mkuu ambapo bila
hivyo chama kingelazimika kuteua mgombea mwingine, hatua ambayo
ingekipotezea sifa na heshima kama chama cha kidemokrasia ya kweli.



Kuokoa jahazi, kiliitishwa kikao cha Kamati Kuu [CC] ya chama kwa
agenda moja tu: “Hali na matarajio ya Uchaguzi wa Rais Visiwani”.
Mwalimu, huku akinukuu taarifa hizo za ki-intelijensia,
aliwatahadharisha wajumbe kwamba, huenda Wakil asingeweza kupata
asilimia 50 ya kura inayotakiwa kushinda katika uchaguzi.

Seif Sharrif Hamad alisikika baadaye akisema, kwa Wakil kukubali kuwania
nafasi hiyo, alikuwa anapiga ngumi ukutani. Akabainisha kwamba, Mwalimu
na Mwinyi walimwita yeye mara tatu kumtaka ampigie kampeni Wakil, hasa
huko Pemba; akaona ilikuwa ni kazi ngumu kumuuza na isiyowezekana.



Alisema, ingawa aliitika wito wa CC kugombea Urais wa Zanzibar
kushindana na Wakil, baadhi ya wajumbe wa NEC [akiwamo Salmin Amour]
waliojiita “Washindi” – [Wakombozi], na yeye kumwita “Mchakazwa”,
hawakuonesha nia njema na maridhiano kwa manufaa ya Zanzibar na
Muungano, huku wakijigamba kwamba, walimweka Wakil kugombea ili
“kuipindua Serikali ya Awamu ya tatu”, kwa maana ya Mwinyi na Hamad, na
ili Zanzibar iweze kutawaliwa kwa staili ya ASP badala ya staili ya CCM.



Ni Abdallah Natepe aliyetafsiri hadharani kuwa hivyo ndivyo
ilivyotakiwa, akisema: “Mapinduzi ya 1964 yalikusudia kumkomboa Mwafrika
Mweusi; lakini Serikali ya Mwinyi na CCM Visiwani inataka kuturejesha
utumwani.



Akaongeza akisema: “Siwezi kukubaliana na mwanachama yeyote wa zamani
wa Zanzibar Nationalist Party [ZNP], Zanzibar and Pemba Peoples Party
[ZPPP] au Umma Party [UP], kwa sababu hawa ni maadui wanaotaka kulipa
kisasi dhidi yaASP”.



Ilikuwa wazi kuwa Natepe alikuwa anasumbuliwa na mzimu wa watu wa kale ASP; ZNP na UP.

Nyerere, huku akionesha kuchukizwa dhahiri na kauli ya Natepe,
alimwambia kwa ukali: “Najua, wewe ni kiongozi [ring leader] wa njama
hizi; una kundi lako, najua!.Lakini elewa kwamba, nchi hii ni ya
Watanzania wote; ubaguzi na udikteta wa kale hauwezi kuvumilika; chunga
ulimi wako!”.



Kisha Mwinyi akaingia kuokoa jahazi alipomshambulia Natepe kwa maneno
makali kwa kuendekeza na kuendesha ubaguzi wa rangi. Na katika hotuba
yake ya kufunga kikao Nyerere alipoza moto kwa kusema: “Nataka muelewe
kwamba, nawaelewa vizuri vijana hawa [Frontliners]; ni vijana wakweli,
wasiovumilia wala kuishi kwa majungu, uzushi na ubaguzi; sio wasaliti.
Sitavumilia kuona wakitendewa kama maadui ndani ya nchi yao”.



Lakini Ali Mzee wa kambi ya Natepe alikuwa jasiri vya kutosha kuomba
maridhiano ili mambo yaishe, na kwamba, Chama katika ujumla wake,
kimuunge mkono Wakil. Kwa uamuzi huo, iliazimiwa kuundwe kikosi cha
kampeni kumsaidia Wakil, kilichojumuisha Mwalimu Nyerere, Ali Hassan
Mwinyi, Rashid Kawawa, Salim Ahmed Salim na Seif Shariff Hamad.



Katika mikutano yote ya hadhara, viongozi hao watano walilaani kundi
la “Wakombozi” [Liberators] kwa kuwaita wanafiki na wachochezi; huku
Kawawa na Mwinyi wakiwahakikishia Wazanzibari kwamba ni sera za CCM
pekee ndizo zitakazowaongoza Wazanzibari, na kwamba ASP kilishakufa;
kwamba wale wote wanaoishi kwa kuongozwa na mzimu wa ASP [Liberators] ni
maadui wa Wazanzibari na wa Muungano, wanaotaka kuirejesha Zanzibar
kwenye enzi za udikteta wa ASP.



Mwalimu kwa upande wake, aliwashambulia kambi ya “Liberators”
akisema: “Msiwasikilize hao, ni watu mfilisi kisiasa; ni masalia ya
udikteta wa kale katika Zanzibar huru inayosonga mbele”, wakataeni,
hawafai”.



Na pale matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar yalipotangazwa,
Oktoba 1985, Wakil alikuwa amepita kwa ushindi duni wa asilimia 58.6 ya
kura zilizopigwa, huku wengi wa wagombea wa Baraza la Wawakilishi wa
mrengo wa “Liberators” wakiwa wameshindwa vibaya.



Mwinyi alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, na Wakil
akajaza nafasi ya Rais wa Zanzibar;Seif Shariff Hamad akabakia Waziri
Kiongozi, pengine kama suluhisho la Wakil kwa kambi mbili hasimu,ya
“Liberators” na “Frontliners”.



Visiwani, migogoro ya kisiasa haiishi, tangu harakati za kupigania
uhuru miaka ya 1950 hadi sasa. Hivyo, vita ya kupigania ukuu ndani ya
CCM kati ya makundi hasimu ya “Liberators” na “Frontliners” ilivaa sura
mpya baada ya baadhi ya “Frontliners” kubadili kambi kwa kujiunga na
kambi ya “Liberators”.Baadhi ya hao walikuwa ni Adam Mwakanjuki, Isaac
Sepetu na Ali Ameir. Kambi ya “Frontliners” ilidhoofu na kuvunjika moyo.



Pigo zaidi kwa kambi hiyo lilikuja pale kundi la “Liberators”
lilipoanzisha kampeni dhidi ya Dk. Salim Ahmed Salim ingawa hakuwa na
mahusiano ya moja kwa moja na “Frontliners”; kukaibuka vita ya kutafuta
“mchawi” na hasira kutawala kwenye mikutano mingi; huku kila kundi
likitafuta mbinu za kulipa kisasi kwa uhasama wa kale.



Hatimaye kundi la “Liberators” ambao walikuwa wengi kwenye NEC ya CCM
liliibuka washindi. Hii ilikuwa dhahiri kwenye uchaguzi waNEC, ambapo
Seif Shariff Hamad alipita kwa mbinde kuwa Mjumbe wa NEC, lakini
akapoteza nafasi ya Ujumbe wa Kamati Kuu [CC], kuashiria kuanza kwake
kuwekwa pembeni kwa nafasi za Chama na Serikali.



Mara Wakil akavunja Serikali ya Zanzibar lakini bila kuvunja Baraza
la Wawakilishi;na wakati huohuo akawateua Makatibu Wakuu wa Wizara
kusimamia na kuongoza shughuli za Serikali. Na alipoteua Baraza jipya la
Mawaziri, Hamad na wenzake wa kambi ya “Frontliners”, walipoteza nafasi
zao. Seif Sharrif Hamad akawa ametunguliwa Zanzibar.



Kana kwamba hilo halikutosha, mwaka mmoja baadaye, kikao cha CCM
kiliitishwa Kizota, Dodoma ambapo Hamad, Shaaban Mloo, Ali Haji Pandu,
Khatib Hassan, Soud Yusuf Mgeni, Hamad Rashid na wengine, walifukuzwa
kwenye chama na hivyo kukamilisha anguko la kishindo la Hamad na wenzake
hao.



Kwa kufanya hivyo, CCM kilidhani kundi hilo limekatwa miguu na ulimi,
kwamba sasa kingeweza kuendesha mambo yake kwa amani na utulivu, lakini
ukweli ilikuwa ni kinyume chake kwa sababu kitendo hicho kiliwafanya
waungane na kujipanga upya kuweza kutoa upinzani mkubwa nje ya Chama na
Serikali.

Muungano wa kundi hili lililoonekana kama “Wasaliti” wa chama, lilitia
hofu kwa Serikali dhaifu Visiwani na kusababisha Hamad na wenzake
kukamatwa na kutiwa kizuizini, kisha wakashtakiwa kwa kosa la uhaini, la
kutaka kupindua Serikali ya Zanzibar.



Na baada ya milolongo mirefu ya kisheria, hatimaye Hamad na wenzake
waliachiwa huru na Mahakama kwa hoja kwamba tuhuma za kutakakupindua
Serikali zilikuwa hazina mashiko kwa sababu Zanzibar si nchi wala dola
inayoweza kupinduliwa.



Kutiwa kizuizini kwa Hamad na kundi lake hakukuwaogofya, badala yake
kuliwakomaza kisiasa kuwa wanamageuzi waliokubuhu. Kwa ujasiri mkubwa na
kujiamini, walianzisha Umoja wa upinzani wa chini kwa chini
uliojulikana kama “Kamati ya Mwelekeo wa Vyama huru” – KAMAHURU; kwa
lengo la kuimarisha demokrasia kisiasa Visiwani. Kufikia hapo, upepo wa
kisiasa ukaanza kuvuma kuelekea kwao.



KAMAHURU kilibadili jina na kuitwa “Zanziabar United Front” [ZUF],
Chama ambacho kufuatia kufunguliwa milango kwa Vyama vingi nchini,
ZUFkiliungana na Chama cha Bara kilichoitwa “Chama cha Wananchi”
[CCW],Mei 1992, kuunda Chama kipya kijulikanacho kama “Civic United
Front” [CUF], na Mwenyekiti wake wa kwanza alikuwa James Mapalala na
kufuatiwa na Musobi Mageni; wakati wote huo Hamad akiwa Makamu
Mwenyekiti na Shaaban Mloo, Katibu Mkuu, nafasi ambayo sasa inashikiliwa
na Hamad.



Kufurukuta kwa Seif Shariff Hamad kutoka Waziri wa Elimu Visiwani
mwaka 1977 hadi kuwa Waziri Kiongozi na kutunguliwa mwaka 1985; na
kutoka “Haini” na Habusu kwa miezi 30, hadi Kiongozi wa Chama cha
upinzani [CUF] chenye nguvu na yeye kushika nafasi ya Makamu wa kwanza
wa Rais wa Zanzibar, ni safari ndefu yenye mabonde na milima inayohitaji
ujasiri na moyo wa aina yake.



Kwa namna siasa za upinzani zinavyoenda Visiwani, inatukumbusha
mitafaruku na uhasama wa kale, kati ya Vyama vya “Zanzibar Nationalist
Party” [ZNP] na ASP; ambapo CUF kinaonekana kuchukua nafasi ya
ZNPtofauti tu kwamba CUF ni cha kitaifa [Tanzania], na CCM kuchukua
nafasi ya ASP. Ilivyo huko Visiwani, CCM Zanzibar ni tofauti na CCM
Bara; na vivyo hivyo CUF Zanzibar na CUF Bara, kwa sababu ya tamaduni na
mazingira tofauti ya kisiasa.



Ni Rais wa Awamu ya Sita wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amani
Abeid Karume, wakati akiteta na Hamad, aliuliza: “Mwenzangu, hadi lini
nchi yetu [Zanzibar], tutaiongoza kwa misingi ya historia ya uhasama wa
kisiasa wa kale? Tunataka tuwarithishe nini watoto [wetu] wa Kizanzibari
chini ya uhasama huu?”.



Majibu ya maswali haya ndiyo yaliyozaa wazo la kuundwa kwa Serikali
ya Umoja wa Kitaifa [SUK] Visiwani, ambayo Hamad ni Makamu wa kwanza wa
Rais.Na kwa sababu hiyo, huenda busara za Karume na Hamad, zimekuwa
chachu na sehemu ya suluhisho la siasa za uhasama zilizoigawa jamii ya
Kizanzibari kwa miaka mingi.





Je, sasa tuamini kwamba, kitendo cha baadhi ya wafuasi wa CUF, cha
kupeperusha bendera za ASP kwenye mikutano yao, ni wito wa Chama hicho
kwa Wazanzibari kuungana chini ya nembo ya Uhuru wa Zanzibar kwa ajili
ya Wazanzibari, bila kujali itikadi zao za kisiasa?

Lakini, swali lingine la kujiuliza ni hili; Wanaungana dhidi ya nani?

Chanzo: Raia Mwema

0 comments:

Post a Comment