Ikulu ya Marekani (White House) imesema katika ripoti
iliyotumwa katika Kongresi ya nchi hiyo kwamba Wamarekani milioni 50
ambao ni sawa na asilimia 15 ya jamii ya watu karibu milioni 300 wa nchi
hiyo, wanaishi katika umaskini.
Ripoti hiyo ya White House pia imesema
kuwa tabaka la kati la raia wa nchi hiyo linasumbuliwa na mbinyo na
mashinikizo kutokana na kutoongezeka mishahara licha ya kuboreka hali ya
uchumi wa Marekani katika miaka ya baada ya mdororo mkubwa wa kiuchumi.
Wakati huo huo taasisi moja ya utafiti ya Ufaransa
ilitangaza hivi karibuni kuwa, Marekani inashika nafasi ya kwanza kati
ya nchi zilizoendelea kwa kuwa na idadi kubwa na watu maskini.
Mstari wa umaskini nchini Marekani ni pato la dola elfu 23
na 850 kwa mwaka kwa familia yenye watu wanne na inasemekana kuwa,
aghlabu ya Wamarekani wenye umri wa kati ya miaka 25 hadi 75 huonja
shubiri ya umaskini kwa miaka kadhaa.
Kiwango cha umaskini huo huwa
shadidi zaidi kwa Wamarekani weusi wenye asili ya Afrika na familia
zenye mzazi mmoja.
Takwimu mpya na rasmi za serikali ya Marekani zinaonesha
kuwa, asilimia 16 ya watoto wa Kimarekani wanaishi chini ya mstari wa
umaskini.
Katika ripoti yake ya hivi karibuni, Kituo cha Takwimu cha
Marekani kilitangaza kuwa, idadi ya watoto wa Marekani ambao familia zao
zinatumia vibali maalimu vya msaada wa chakula kutokana na umaskini wa
kupindukia, imeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka saba
iliyopita.
Wakati huo huo Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa
(UNICEF) limetangaza kuwa Marekani inashikilia nafasi ya pili kati ya
nchi zinazoongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watoto maskini kati
ya nchi zilizoendelea.
Vilevile ripoti mpya ya jumuiya isiyo ya
kibiashara ya "Elimu na Malezi Kusini" ya huko huko Marekani inasema
zaidi ya nusu ya wanafunzi wanaosoma katika shule za serikali
wanastahiki kupewa msada wa chakula na mahitaji mengine ya kimaisha au
kwa bei ya ruzuku.
Ripoti ya jumuiya hiyo inasema thuluthi mbili ya
majimbo ya kusini mwa Marekani inakabiliwa na umaskini mkubwa ulioenea
kati ya wanafunzi.
Licha ya ripoti hizo zote zinazoonesha kiwango kikubwa cha
umaskini nchini Marekani lakini serikali ya nchi hiyo imezidisha
mazingatio yake kwenye miradi yenye gharama kubwa ya kijeshi na kijasusi
ndani na nje ya nchi hiyo.
Gazeti la Financial Times la Marekani
limeandika kuwa nchi hiyo ilitumia zaidi ya dola trilioni mbili na
bilioni 700 katika vita vya Afghanistan na Iraq.
Hii ni katika hali
ambayo bajeti ya mwaka 2014 ya Marekani ilikuwa dola trilioni 3 na
bilioni 77.
Bajeti ya masuala ya kijeshi ya Marekani katika mwaka huu wa
2015 ni dola bilioni 585.
0 comments:
Post a Comment