Nov 26, 2014

Maombi Ya Sheikh Farid Yaanza Kusikilizwa

IMG_0030

MAHAKAMA KUU ya Tanzania, imeanza kusikiliza maombi ya Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheikh Farid Hadi Ahmed (43) na wenzake waliyoomba Mahakama ipitie kesi ya awali inayowakabili.

Kusikilizwa kwa maombi hayo, kunatokana na mashtaka ya kula njama ya kuingiza watu nchini, kushiriki vitendo vya ugaidi pamoja na kusaidia kufanyika kwa vitendo hivyo.

Maombi hayo yalisikilizwa jana, mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk Fauzi Twaib, Wakili wa Serikali, Peter Njike akisaidiana na George Barasa.

Awali wakili wa utetezi, Abubakar Salum alidai kwamba wanaiomba Mahakama itoe tafsiri, kwanini watu wawili walioingizwa nchini kufanya vitendo hivyo, hawafikishwi mahakamani, pia ni raia wa nchi gani, huku mashitaka hayo yakiwa hayaonyeshi lini na eneo gani vitendo hivyo vimefanyika.

Kwa upande wa wakili wa serikali, Njike aliiomba Mahakama impe nafasi ya kusikilizwa, kwa kuwa upande wa Jamhuri ulikosa majibu kutokana na maombi hayo kufikishwa kwa hati ya dharura.

Baada ya kupewa nafasi ya kusikilizwa, Njike aliiomba Mahakama ipange tarehe nyingine ili apate muda wa kutoa majibu kuhusu maombi hayo, Jaji Twaib aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 4, mwaka huu ili upande wa Jamhuri uweze kutoa majibu.

Hata hivyo, Jaji Twaib alisema kama upande wa Jamhuri utakuwa na jambo la ziada kuhusu maombi hayo yanayotakiwa kufikishwa Novemba 28, mwaka huu huku upande wa utetezi kama wana jambo la ziada walifikishe Desemba 1, mwaka huu.

Mbali na Farid, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na mashtaka hayo ni Nassoro Hamad, Hassan Bakari, Ahtari Humoud, Mohamed Isihaka, Abdallah Hassan, Hussein Mohamed, Juma Sadala na Said Kassim. 

Wengine ni Khamis Amour, Abubakar Abdallah, Salum Ali, Salum Amour, Alawi Othman, Rashid Ally, Amir Khamis, Kassim Salum na Said Shehe.

Kesi inayowakabili inadaiwa kuwa kati ya Januari 2013 na Juni mwaka huu washtakiwa hao kwa pamoja walipanga njama ya kutenda makosa hayo ya kula njama za kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo vya kigaidi.

0 comments:

Post a Comment