Sep 3, 2014

SHEIKH PONDA AIOMBA MAHAKAMA ITUMIE BUSARA

Sheikh Ponda aiangukia mahakama

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda

KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, ameiangukia Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa kuiomba itumie busara kusimamisha kesi ya uchochezi inayomkabili mkoani Morogoro.

Maombi hayo yaliyokwama mara kadhaa kutokana na sababu za kisheria, yaliwasilishwa jana kupitia wakili wake, Juma Nassoro, wakati rufaa yake ya kupinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyomtia hatiani kwa kuingia kwa jinai katika kiwanja cha Chang’ombe Markaz na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja nje, ikisikilizwa.

Wakili Nassoro akiwasilisha maombi hayo mbele ya Jaji Augustine Shangwa, aliiomba mahakama hiyo isimamishe kesi ya uchochezi inayomkabili Ponda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, hadi itakapotoa uamuzi wa rufaa hiyo.

“Mheshimiwa jaji endapo Mahakama ya Morogoro ikimtia hatiani Ponda na kumhukumu wakati Mahakama Kuu ikikubali hoja zake za rufaa na kutengua hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, itaishushia hadhi mahakama.

“Mahakama ikisimamisha kesi ya Morogoro, upande wa Jamhuri hautaathirika kwa kuwa ndio waliofungua kesi, naomba mahakama yako tukufu itumie busara kusimamisha kesi hiyo,” alidai Nassoro.

Katika rufaa hiyo, Ponda anadai hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani kwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.

Ponda na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama, wizi wa mali yenye thamani ya Sh milioni 59.6 na kuingia kijinai kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali eneo la ardhi inayomilikiwa na Kampuni ya Agritanza Ltd na uchochezi.

Katika hukumu iliyotolewa Mei 9, 2013, Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa wa Mahakama ya Kisutu alimtia hatiani Ponda peke yake kwa kosa la kuingia kijinai katika eneo la Agritanza Ltd, na ikawaachia huru washtakiwa wengine wote.

Jaji Shangwa aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 10, mwaka huu kwa ajili ya upande wa Jamhuri kujibu hoja za Sheikh Ponda.

0 comments:

Post a Comment