Sep 2, 2014

CUF kuandamana siku tatu kupinga Bunge la Katiba

Makamu mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji akoinyesha waraka wa siri wa CCM unaodaiwa kuandaliwa kwa ajili ya Rasimu ya Katiba inayojadiliwa Dodoma, alipokuwa akifungua kongamano la wanachama wa chama hicho, Buguruni jijini Dar es Salaam juzi

Chama cha Wananchi (CUF) kitafanya maandamano ya siku tatu za kazi kupinga kuendelea kufanyika kwa vikao vya Bunge la Katiba ambayo yatafanyika katika mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam.

Maandamano hayo ni mwendelezo wa hatua ambazo zimekwishachukuliwa na chama hicho pamoja na vyama vingine vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Aprili 16, mwaka huu, wajumbe kutoka vyama vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi vinavyounda Ukawa walitoka nje ya Bunge wakidai kuchakachuliwa kwa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko la Katiba.
Jana, uongozi wa CUF uliitisha kongamano la wanachama wake ili kuwauliza nini kifanyike baada ya wajumbe wa chama hicho kutoka nje ya Bunge lakini chombo hicho kikapuuza madai yao. 

Kongamano hilo lilifunguliwa na makamu mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji ambaye aliongoza kongamano hilo hadi maazimio hayo yalipotolewa.
Akisoma maazimio ya wanachama baada ya kutoa maoni yao, ofisa uchaguzi wa CUF, Abdulrahman Lugone alisema wanachama wengi wameazimia maandamano yafanyike kwa siku tatu katika Mkoa wa Dodoma na yaishie katika majengo ya Bunge.
“Tunataka maandamano haya yafanyike katika siku za kazi ili kupeleka ujumbe mzito kwa jamii kwamba maoni yao ndiyo msingi mkuu wa Katiba,” alisema katika kongamano hilo lililofanyika katika makao makuu ya chama hicho Buguruni wilayani Ilala.
Alisema pia maandamano hayo yatafanyika siku hiyo hiyo mkoani Dar es Salaam na kuishia kwenye ofisi ndogo za Bunge ambako kuna ofisi nyingi za Serikali.
“Tunaomba wafanyakazi na wananchi wanaopinga kuendelea kufanyika kwa vikao vya Bunge hilo watuunge mkono kwa kushiriki katika maandamano haya,” alisema.
Lugone alisema vyama vingine vinavyounda Ukawa vinaombwa siku za maandamano zitakapotangazwa kusitisha shughuli zao ili wafuasi wake waweze kushiriki kwenye maandamano hayo.
Alisema makao makuu ya chama hicho yanaratibu maandamano hayo na kwamba wafuasi wa chama hicho watatangaziwa tarehe ya kufanyika. 

Wakati kongamano hilo linaendelea makao makuu ya CUF, nje ya uzio kulikuwa na polisi zaidi ya 25 waliokuwa kwenye magari matatu.
ambao walifika kuanzia saa 5.00 asubuhi na kuondoka saa 7.30 mchana baada ya kumalizika kwa kongamano hilo.
Akifungua kongamano hilo, Duni ambaye pia ni Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar, alisema Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta ameonyesha udhaifu mkubwa katika kukiongoza chombo hicho.

0 comments:

Post a Comment