Jul 3, 2014

Waislamu China wazuiwa kufanya ibada Ramadhani

Serikali ya China imewapiga marufuku Waislamu katika jimbo la Xinjiang lililoko kaskazini magharibi mwa nchi hiyo kutekeleza shughuli na harakati zozote za kidini hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Taarifa zinasema kuwa, wakati Waislamu wakipigwa marufuku kukusanyika na kufanya ibada kwenye Misikiti katika mwezi huu mtukufu, Chama cha Kikomonisti  kinaendesha vikao vyake kwenye misikiti iliyoko jimboni humo. 

Serikali ya China inadai kwamba, Waislamu wamekuwa wakizitumia shule na idara za serikali kwa kutoa mahubiri na mafundisho ya dini ya Kiislamu. 

Taarifa zinasema kuwa, baadhi ya mameneja wa viwanda vya Kichina wanawapiga marufuku Waislamu kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani, kwa madai kuwa wanasababisha kushuka uzalishaji kwenye viwanda katika jimbo hilo.

Jimbo la Xinjiang ambalo wakazi wake wengi ni Waislamu linatuhumiwa na serikali ya China kuwa linataka kujitenga, jambo ambalo linasababisha mapigano ya mara kwa mara kati ya jeshi la polisi na wakazi wa jimbo hilo. 

Hivi karibuni Mahakama ya Xinjiang iliwahukumu watu 113 vifungo vya kuanzia miaka 10 hadi maisha jela, kwa tuhuma za kushiriki kwenye ghasia na machafuko jimboni humo.    

0 comments:

Post a Comment