Jul 4, 2014

Uganda yasema haitishwi na vikwazo vya kupinga mapenzi ya jinsia moja

Gazeti la Red Cross lilichapisha majina ya watu wanaoshukiwa kuwa wapenzi wa jinsia moja baada ya sheria kupitishwa
Katibu mkuu wizara ya mambo ya nje wa Uganda, Balozi James Mugume, amesema kuwa Uganda haitishwi na vikwazo ilivyowekewa na Marekani kama hatua ya kupinga sheria yake kali kuhusu mapenzi ya jinsia moja.

Mwandishi wa BBC mjini Kampala, Isaac Mumena anasema kuwa Balozi Mugume ameelezea kuwa serikali ya Uganda hata hivyo itafanya mazungumzo na Marekani ili kufafanua hatua waliyochukua.
Amesisitiza kuwa wataieleza Marekani sheria hiyo inapinga tabia ambayo sio ya kiafrika na maadili ambayo hayakubaliki katika jamii nyingi za kiafrika.

Serikali imesisitiza kuwa vikwazo hivyo havitakuwa na athari kubwa kwa nchi hiyo na pia imekanusha madai ya mashirika ya kijamii kuwa tayari sheria hiyo imechochea ongezeko la dhuluma dhidi ya wapenzi wa jinsia moja.

Vikwazo vyenyewe ni pamoja na kufutilia mbali msaada wa kijeshi, kuwapiga mrufuu baadhi ya maafisa wa serikali kusafiri nje na kupiga tanji mali zao.
Maandamano kupinga mapenzi ya jinsia mopja na kumpongeza Rais Museveni kuwa kupitisha sheria hiyo

Kadhalika msemaji wa serikali Ofwono Opondo amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kuwa wananchi wa Uganda wanafahamu kuwa hawatategemea tena msaada wa nchi za Magharibi

Sheria hiyo iliyotiwa saini na Rais Yoweri Museveni mwezi Februari inasema kuwa wanaopatikana na hatia mara mbili ya kuhusika na mapenzi ya jinsia moja watafungwa maisha jela.

Sheria hiyo pia inaharamisha vitendo vya mapenzi ya jinsia moja pamoja na kuwataka wananchi kuwashitaki watu wanaohusika na vitendo vya mapenzi ya jinsia moja kwa maafisa wakuu.

Ikulu ya White house imelaani sheria hiyo ikisema kuwa inakwenda kinyume na uhusiano kati ya nchi hizo ikitoa wito wa sheria hiyo kufutuliwa mbali. 

Waziri wa mambo ya nje John Kerry, amefananisha sheria hiyo na sheria za utawala wa zamani wa kinazzi nchini Ujerumani.

0 comments:

Post a Comment