Jul 3, 2014

Mwakyembe awafukuza wafanyakazi 13 JNIA

mwakyembe Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu uamuzi wake wa kuwafukuza wafanyakazi 13 wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).



Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe amewatimua wafanyakazi 13 wa wizara tatu waliokuwa wakifanya kazi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam kwa kujihusisha na vitendo vya kupokea rushwa kutoka kwa raia wanaotoka nje ya nchi.

Wafanyakazi waliotimuliwa ambao walipewa muda hadi saa 6:00 mchana jana wawe wameondoka katika uwanja huo wanatoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Wizara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mifugo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwakyembe aliwataja wafanyakazi hao kuwa ni Teddy Mwasenga, Ester Kilonzo, Rehema Mrutu, Mary Kadokayosi, Kisamo Samji, Anneth Kiliyanga ambao wanatoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.

Wafanyakazi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ni Agness Shirima, Hamis Bora, Valeri Chuwa, Elingera Mghase na Remedius Kakulu na watumishi wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ni Eshi Samson Ndosi na Anne Setebe.

Alisema amechukua uamuzi huo baada ya hivi karibuni kupokea malalamiko kutoka kwa abiria hasa wanaotoka nchi za kiarabu, India na China kwamba wanakaguliwa sana tofauti na abiria kutoka nchi nyingine.

Alisema mfano maofisa wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika wanawalenga Wachina, Wahindi na Waarabu kwa kuwanyang’anya bidhaa zao za madawa na vyakula kwa madai haziruhusiwi kuingia nchini.

“Ni kweli wafanyakazi hao wana wajibu mkubwa kukagua, lakini kinachotia mashaka wageni wakishatoa tu hongo wanarejeshewa mizigo yao na wale ambao wanashindwa kutoa chochote bidhaa zao zinachukuliwa, hatujawaweka watu uwanjani kuchukua rushwa,” alisema.

Alisema katika hali ya kushangaza bidhaa hizo za wageni wanazozichukua watumishi wa wizara hiyo wanazipeleka majumbani kwao na hali inayotia mashaka ni kwanini bidhaa ambazo ni haramu zinageuka kuwa halali kwenye matumbo yao.

Dk. Mwakyembe alisema wafanyakazi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi nao wanajihusisha na vitendo kama wenzao wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.

Kwa upande wa wafanyakazi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, alisema wanalalamikiwa kwa kuwalenga Wachina na Wahindi kwa kuwadai kadi ya chanjo ya homa ya manjano na kwamba abiria wasiokuwa na kadi hizo wanatozwa fedha kati ya Dola za Marekani 50 hadi 100.

Kwa mujibu wa utaratibu uliopo, kila mgeni anayefika uwanjani hapo lazima awe amepata chanjo hiyo, vinginevyo hulazimika kupewa uwanjani hapo kwa kulipia.

Alisema amechukua hatua hiyo baada ya kupitia ushahidi wote wa kamera za kiusalama za CCTV zilizopo uwanjani hapo na ushahidi mwingine wa maandishi dhidi ya vitendo viovu vinavyofanywa na wafanyakazi wa wizara hizo.

Dk. Mwakyembe alisema watumishi hao hawatakiwi tena kufanya kazi JNIA na watarejea katika wizara zao ambako watakwenda kuchukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na utovu wa nidhamu waliofanya.

“Kutokana na ushahidi wa kamera za CCTV na wa maandishi, naagiza watumishi wa wizara hizo ambao wapo JNIA sitaki kuwaona katika uwanja huo kuanzia leo (jana) saa 6:00 mchana na nimeagiza wasindikizwe na polisi,” alisema.

Aidha, wafanyakazi wengine waliobaki wa wizara hiyo kuanzia sasa wawe wanavaa sare kama ilivyo kwa maofisa wa Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi au wavae reflekta na kama hawataki waondoke.

Alisema viwanja vya ndege vina nafasi kubwa katika kujenga na kulinda heshima ya nchi katika jumuiya ya kimataifa, hivyo mgeni akikumbana na mambo ya ovyo ovyo kwenye viwanja hivyo atajenga taswira mbaya na kama ni mwekezaji anaanza kufikiria kupeleka uwekezaji wake katika nchi nyingine.

Dk. Mwakyembe alisema wafanyakazi wote wa viwanja vya ndege ni lazima watambue kuwa wao ni mabalozi wa nchi katika kulinda heshima ya nchi yetu hivyo wanatakiwa kufanya kazi kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.

MAJIBU YA WIZARA
Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja, alipoulizwa alisema kwa kuwa Dk. Mwakyembe amezungumza hayo jana wanasubiri taratibu zifuatwe ndipo hatua za kuchukua dhidi ya watumishi wa wizara hiyo zifuatwe.


“Kama amesema leo (jana) serikali ina taratibu zake tunasubiri itakapoletwa taarifa taratibu nyingine zitafuata,” alisema.

Kwa upande wa Msemaji wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mohamed Bahari, alisema wizara itakapopata barua rasmi kutoka Wizara ya Uchukuzi, itaitisha mafaili ya wafanyakazi hao na kuangalia hatua za kuwachukulia.

Msemaji wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Richard Kasuga, alisema watumishi wa wizara hiyo watakaobainika walijihusisha na vitendo hivyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za umma.

“Dk. Mwakyembe ni waziri wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hiyo kwa kuwa ameshasema hao watumishi watashughulikiwa maana kila mtumishi wa umma anastahili kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo,” alisema

 47683093

0 comments:

Post a Comment