Jul 6, 2014

Kiongozi wa Ikhwan Misri ahukumiwa maisha jela

Mohammad Badie akiwa kwenya seli kortini mjini Cairo Mohammad Badie akiwa kwenya seli kortini mjini Cairo
Mahakama ya Misri imemhukumu kifungo cha maisha kiongozi wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin, Mohammad Badie. 



Taarifa kutoka Cairo zinasema kuwa Badie na wanachama wengine 36 wa harakati hiyo wamehukumiwa kifungo cha maisha gerezani huku mahakama hiyo ikithibitsha hukumu ya kifo dhidi ya wanachama wengine 10 wa Ikhwan ambao wengi wao bado wanasakwa na vikosi vya usalama. Mahakama hiyo imedai kuwa Badie alisababisha vifo katika maandamano yaliyoitishwa mwaka jana kulalamikia hatua ya jeshi kumpindua rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia Misri Mohammad Morsi. 

Ikumbukwe kuwa mwezi uliopita wa Juni mahakama nyingine ya Misri ilithibitsha hukumu ya kifo dhidi ya Badie na wanachama wengine 180 wa Ikhwanul Muslimin. 

Baada ya jeshi kumpindua Morsi mwezi Juni mwaka jana, maelfu ya wafuasi wa Ikhwanul Muslimin waliandamana kote Misri ambapo vikosi vya usalama vilitumia mkono wa chuma kukandamiza maandamano hayo na kupelekea karibu watu 2,000 kupoteza maisha. 

Rais Abdul Fatta el-Sisi ambaye akiwa mkuu wa jeshi aliongoza mapinduzi dhidi ya Morsi alichaguliwa kuwa rais wa Misri mwezi Mei na hapo akatangaza azma yake ya kuangamiza Harakati ya Ikhwanul Muslimin. 

Harakati hiyo iliyoanzishwa mwaka 1928 ilipigwa marufuku kwa miongo kadhaa kabla ya kuibuka katika mwamko wa Kiislamu mapema mwaka 2011 uliopelekea kupinduliwa dikteta Hosni Mubarak.

0 comments:

Post a Comment