Jul 31, 2014

17 wafa papo hapo

 
Wananchi wakiangalia mabaki ya basi la Kampuni ya Morobest baada ya kupata ajali katika Kijiji cha Pandambili wilayani Kongwa jana.

Watu 11 kati ya 17 waliofariki dunia papohapo katika ajali eneo la Pandambili wilayani Kongwa, Dodoma wametambuliwa na wanne kati yao tayari wamechukuliwa na ndugu zao.

Ajali iliyosababisha watu 56 kujeruhiwa vibaya. iliyahusisha magari mawili ambayo ni basi aina ya Scania mali ya Kampuni ya Morobest lililokuwa likitokea Mpwapwa kwenda Dar es Salaam, ambalo liligongana na uso kwa uso na lori lenye tela, lililokuwa limepakia shehena ya mabomba.
Ajali hiyo ambayo ilisababisha vifo vya madereva wa magari hayo, ilitokea meta chache kutoka mahali ilikotokea ajali iliyosababisha kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime, marehemu Chacha Wangwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma David Misime aliielezea tukio hilo lilitokea saa 2 asubuhi kuwa miongoni mwa ajali mbaya ambazo zimetokea mkoani humo katika siku za karibuni.
“Ni watu 17 ambao wamekufa hapa hapa, kati ya hao 12 ni wanaume na wanawake ni watano, majeruhi ni 56, kati yao tisa wana hali mbaya zaidi,” alisema Misime.
Hadi jana jioni maiti za watu kumi na moja walikuwa wametambuliwa na wanne kati yao walichukuliwa na ndugu zao.
Waliotambuliwa ni Gabriel Lemanya (Dereva wa lori) ambaye ni Mkazi wa Ndebwe wilaya ya Chamwino, Said Lusogo (dereva wa basi), Omari Mkubwa (kondakta wa basi) na Mikdadi Zuberi ambaye alikuwa ni utingo wa lori.
Wengine ni Justin Makasi, Gabriel Chiwipe, Marick Masawe na Melina Maliseli, Wilson Sudai (wote wakazi wa Mpwapwa) watu wawili walitambulika kwa jina moja ambao ni Christina (Mpwapwa) na Nasibu mkazi wa Kongwa.
Taarifa zaidi zinasema damu zilikuwa zimetapakaa katika sehemu kubwa ya barabara ilikotokea ajali hiyo na kwamba magari hayo yalikuwa yameharibika vibaya sehemu za mbele. 

Kadhalika baadhi ya mabomba yaliyokuwa kwenye lori yalikuwa yamerushwa umbali wa karibu meta 20 kutoka eneo la ajali.
Mashuhuda walisema Polisi wa Kituo cha Kongwa walifika katika eneo la ajali muda mfupi tu baada ya magari hayo kugongana na kwamba walisaidia kudhibiti usalama wa mali za abiria, zikiwamo simu za mkononi zaidi ya 20 ambazo zilikabidhiwa kwa uongozi wa polisi Mkoa wa Dodoma.
Mashuhuda wazungumza
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Christopher Kangoye ambaye alikuwa kiongozi wa kwanza kufika katika eneo la tukio, alisema chanzo cha ajali hiyo kilikuwa ni uzembe uliofanywa na dereva wa lori ambaye kwa sasa ni marehemu.

0 comments:

Post a Comment