Jun 27, 2014

Al-Shabab wavamia kambi ya kijeshi ya AMISOM na kusababisha vifo vya wanajeshi wawili

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika AMISOM
Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika AMISOM

Makomandoo wa wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al Shabab nchini Somalia wamevamia kambi ya kijeshi ya Umoja wa Afrika nchini Somalia wakiwa wamevalia magwanda ya kijeshi na kuwauwa wanajeshi wawili wa kulinda amani wa AMISOM kutoka nchini Djibouti.

Kundi hilo limethibitisha kuvamia kambi hiyo katika mji wa Bulla Burde, Kilomita 200 kutoka jiji la Mogadishu na kupambana na wanajeshi hao wa Afrika.

Msemaji wa Al Shabab Abdulaziz Abu Musab ameliambia Shirika la Habari la AFP kuwa “Makao Makuu ya majeshi ya Umoja wa Afrika yalivamiwa na wapiganaji wetu na tumewaua wanajeshi sita.,”

Hata hivyo, msemaji wa Majeshi ya AMISOM nchini Somalia Elio Yao, amekanusha madai hayo ya Al Shabab na kusisitiza kuwa, kundi hilo liliwaua wanajeshi wawili wa Djibouti wakati wa mapambano hayo nje ya kambi hiyo.

“Kuliwa na makabiliano ya risasi katika lango la kuingia katika kambi yetu, na wanajeshi wawili kutoka Djibouti waliuliwa....na magaidi hao hawakufanikiwa kuingia katika kambi yetu,” aliongeza.

Wanagambo wa Al Shabab nchini Somalia
Haya ndio mashambulizi ya hivi punde kutekelezwa na kundi la Al Shabab dhidi ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini humo.

Wakaazi wa mji huo wanasema walisikia milio ya risasi wakati wa mapambano hayo kuanzia siku ya Alhamisi asubuhi.

“Kulikuwa na mapambano makali, na mlipuko mkubwa kabla ya kupambazuka,” Ahmed Abdirisak mkaazi wa mji huo alisema.

Mashambulizi mjini Somalia
Mashambulizi ya hivi karibuni ya kundi hili limekuwa likilenga majengo ya serikali lakini jeshi la Umoja wa Afrika linasema linashinda vita hivyo.

Juma hili, jeshi hilo likiongozwa na lile la Kenya  KDF lilisema liliwaua zaidi ya wanamgambo 80 wa Al Shabab Kusini mwa nchi hiyo.

0 comments:

Post a Comment