Kamishna wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Ali Saleh amesema atawashangaa wajumbe wa Baraza
la Wawakilishi Zanzibar (BLW), iwapo watapinga mfumo wa Serikali tatu
uliopendekezwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba.
Akizungumza mwishoni mwa wiki kwenye semina
maalumu ya kujadili rasimu ya pili ya Katiba iliyofanyika kwenye Ukumbi
wa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni na kuhudhuriwa na makamishna
sita wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Zanzibar, alisema mfumo wa
Serikali mbili unaotetewa na CCM umeshindwa kutatua kero za Muungano kwa
miaka 50 iliyopita na hakuna njia mbadala zaidi ya kujiondoa katika
mfumo.
“Nitashangaa sana iwapo wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi Zanzibar wataupinga mfumo wa Serikali Tatu, kwa kuwa muda
mrefu wamekuwa wakizungumza jambo hilo hata kulipendekeza kama ufumbuzi
wa kudumu,” alisema Saleh ambaye kitaaluma ni mwanasheria.
Alisema mambo yasiyokuwamo katika orodha ya mambo
ya Muungano yamekuwa na wakati mgumu kwa miaka 50 na Zanzibar kushindwa
kunufaika moja kwa moja, huku upande wa pili wa Muungano ukinufaika
nayo.
Hata hivyo, Mwakilishi wa Viti Maalumu na Makamu
Mwenyekiti wa UWT Zanzibar, Asha Bakari Makame alisema hakubaliani na
madai ya Saleh kuwa mapendekezo ya wawakilishi ni mfumo unaopendekeza
Serikali tatu.
Asha alisema hakumbuki iwapo wawakilishi waliwahi
kutoa pendekezo la pamoja na kuunga mkono Serikali tatu na kuwa haipaswi
kutiliwa maanani.
“Sikubaliani na dai la Kamishna Saleh…Naomba afute usemi wake na kutuomba radhi,” alisema Bakari.
Alisema hakukuwa na haja ya kuendelea kufanyika
makongamano, warsha wala semina kwa kuwa kazi ya Tume ya Mabadiliko
imegota ukingoni baada ya kukusanya maoni ya wananchi na kuandika Rasimu
ya pili ya Katiba.
0 comments:
Post a Comment