Oct 24, 2013

ZANZIBAR WAGOMEA MTAALA WA ELIMU WA BARA


  
 ALLY JUMA SHAMHUNA,WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI ZANZIBAR
 Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imesema masomo ya dini na mengine, yataendelea kufundishwa pamoja na kufanyiwa mitihani katika ngazi zote.


Alisema wizara hiyo haijakubaliana na waraka wa elimu kutoka Tanzania Bara wa kuyafanya masomo hayo kuwa ya hiari, hivyo yasichangie asilimia yoyote katika ufaulu wa mtahiniwa.Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Abdallah Mzee, ameyasema hayo Zanzibar jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ili kukanusha taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari zikidai Wizara hiyo imeondoa mtaala wa masomo ya dini na Kiarabu kwenye mitihani ya Taifa. 

Alisema watendaji kutoka Wizara ya Elimu Tanzania Bara, walikutana na wenzao wa Zanzibar ili kujadili waraka wa elimu waliokuja nao uliokuwa unataka kufanyike mambo mapya.
Bw. Mzee aliongeza kuwa, katika waraka huo wenzao kutoka Bara walipendekeza masomo ya dini ya Kiislamu, Kikristo, lugha ya Kiarabu, Kifaransa, Kompyuta, muziki yawe ya hiari kwa mwanafunzi kuyasoma na yasisaidie ufaulu wowote katika viwango vya madaraja ya ufaulu. 

"Waraka ulipendekeza masomo hayo yakiwemo dini na Kiarabu yasisaidie chochote katika kupandisha au kushusha vision ya mtahiniwa," alifafanua Bw. Mzee. 
Aliongeza kuwa, ilipendekezwa utaratibu huo mpya uanzwe kufanyiwa kazi kwa wanafunzi ambao wataingia kidato cha kwanza mwaka 2014 na ifikapo 2017, wanafunzi hao wautumie katika kidato cha nne.
Hata hivyo, Bw. Mzee alisema watendaji wa Zanzibar waliupinga utaratibu huo kwa kuwa haukidhi matakwa ya Zanzibar. 

"Watendaji wetu waliupinga waraka huo kwani hautufai na unatofautiana sana na sisi kulingana na hoja zetu tulizotoa, pia walikubali kuurudisha ili usiweze kufanyiwa kazi," alisema. 

Alisema Wizara ya Elimu Zanzibar, inatoa Mchepuo wa Masomo ya lugha katika skuli tofauti ikiwemo Sekondari ya Kiponda hivyo itakuwa vigumu kufuata utaratibu huo. 
 

  Akizungumzia somo la dini, Bw. Mzee alisema somo hilo kwa Zanzibar ni muhimu sana pia ni miongoni mwa masomo yenye walimu wazuri wa ngazi za Stashahada hadi Udaktari-PhD na ufundishwaji wake huanzia darasa la kwanza hadi Chuo Kikuu hivyo kubadili utaratibu isingewezekana. 

  Aliongeza kuwa, katika dunia ya sasa, somo kama kompyuta ni muhimu sana hivyo kulifanya halina ulazima ni kujirudisha nyuma kimaendeleo."Licha ya uhusiano mzuri uliyopo kati ya Wizara yetu na Bara, sisi hatukushirikishwa katika uanzishwaji wa waraka husika," alisema.
Katika hali ya kuliweka sawa jambo hilo, Mawaziri wa Wizara hizo Bw. Ali Juma Shamhuna na mwenzake wa Bara, Dkt. Shukuru Kawambwa, wanatarajia kukutana kesho kulijadili jambo hilo

0 comments:

Post a Comment