Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa
unajiandaa kuwahamisha Waislamu wapatao 19,000 ambao wanakabiliwa na
hatari ya kushambuliwa na wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka huko
Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Fatoumata Lejeune-Kaba Msemaji wa Shirika la
Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) amewaambia waandishi wa
habari huko Geneva Uswisi kuwa, shirika hilo halitaki kuona watu
wakiuliwa.
Amesema kuwa wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka
wanadhibiti njia kuu za kuingilia na kutoka katika mji mkuu Bangui na
pia idadi kadhaa ya miji na vijiji huko kusini magharibi mwa Jamhuri ya
Afrika ya Kati.
Msemaji wa Shirika la Kuhudumia
Wakimbizi la Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa wanamgambo wa Anti-Balaka
ni tishio hasa kwa Waislamu wanaoishi katika kitongoji cha PK 12 huko
Bangui, katika miji ya Boda, Carnot na Berberati huko magharibi mwa
Bangui na mji wa Bassangoa huko kaskazini.
Fatoumata Lejeune-Kaba
amesema kuwa UNHCR iko tayari kusaidia kuwahamishia Waislamu hao
wanaokabiliwa na vitisho vya wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka
katika maeneo salama ndani au nje ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
0 comments:
Post a Comment