Mar 28, 2014

Waislamu Myanmar waendelea kunyanyaswa

Mamia ya maelfu ya wananchi na watawa wa Myanmar jana walifanya maandamano wakiishinikiza serikali kutowapatia Waislamu wa Rohingya haki ya uraia wa nchi hiyo.
 Taarifa zinasema kuwa, zaidi ya watu laki mbili wa jimbo la Rakhine wakiwemo watawa walifanya maandamano hayo katika mji wa Yangon, wakiitaka serikali isitoe kibali cha kupewa uraia Waislamu wa Rohingya na wala wasihesabiwe kwenye zoezi la sensa linalotarajiwa kufanyika hivi karibuni nchini humo. 

Serikali ya Myanmar imepanga kutekeleza zoezi la sensa ya watu mwanzoni mwa mwezi ujao wa Aprili, ikiwa ni sensa ya kwanza kufanyika nchini humo baada ya kupita zaidi ya miongo mitatu. 

Inafaa kuashiria hapa kuwa, tokea nchi hiyo ijipatie uhuru mwaka 1948, Waislamu wamekuwa wakiteswa na kukandamizwa. 

Serikali ya Myanmar mara kwa mara imekuwa ikikosolewa vikali na makundi ya kutetea haki za binadmu kwa kushindwa kuwalinda Waislamu wa Rohingya ambao wamekuwa wakiuawa na kuchomewa moto nyumba zao na Mabudha wenye misimamo mikali nchini humo.

0 comments:

Post a Comment