Feb 14, 2014

Watu 7 wauawa katika mlipuko wa bomu Somalia

Watu saba wameripotiwa kuuawa katika mripuko wa bomu la kutegwa ndani ya gari, karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mogadishu, mji mkuu wa Somalia. 

Kamanda wa jeshi la polisi Abdul-Qadir Ahmad amesema kuwa, gari iliyokuwa na mada za miripuko iliripuliwa kwa rimoti ya mbali karibu na uwanja huo wa kimataifa eneo ambalo wanaishi wanadiplomasia wengi wa kigeni. 

Kwa mujibu wa Abdul-Qadir Ahmad watu 15 wengine wamejeruhiwa katika mripuko huo sanjari na kusababisha uharibifu mkubwa kwa magari yaliyokuwa karibu na eneo la tukio. 

Tayari kundi la wanamgambo la ash-Shabab limetangaza kuhusika na shambulio hilo. 

Siku chache zilizopita kundi la ash-Shabab lilitekeleza shambulizi mjini Mogadishu na kupelekea watu watano kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa, akiwemo Ahmad Omar Mudan msaidizi wa mkuu wa mkoa wa Shabelle  aliyekatika mkono na mguu kufuatia shambulio hilo la bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari lake.

0 comments:

Post a Comment