Feb 14, 2014

Mary Wambui avuliwa ubunge nchini Kenya

Mbunge wa Othaya nchini Kenya amepoteza nafasi yake bungeni baada ya mahakama ya rufaa kuamua kwamba hakuchaguliwa ki halali. 
Bi. Mary Wambui alitangazwa kuwa mshindi baada ya kuwashinda wapinzani wake kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Machi 4 mwaka jana.
Majaji 3 waliosikiliza kesi iliyowasilishwa na mpinzani wa Wambui wamesema sheria nyingi za uchaguzi zilikiukwa kwenye uchaguzi wa eneo bunge la Othaya mwaka uliopita na kwa mantiki hiyo wamelazimika kufutilia mbali matokeo yake. 

Awali mahakama kuu ilikuwa imeamua kwamba, matatizo yaliyojitokeza kwenye uchaguzi huo yalikuwa madogo na hayangeweza kuathiri matokeo jumla ya uchaguzi wa Othaya. 

Hata hivyo, mlalamikaji kwenye kesi hiyo, Peter King’ara aliamua kukata rufaa na amepongeza uamuzi wa mahakama ya rufaa akisema haki imetendeka.

Wambui ameilaumu familia ya rais mustaafu Mwai Kibaki kutokana na masaibu yake. 

Itakumbukwa kwamba, rais mustaafu alikuwa akimuunga mkono mpinzani wa Wambui wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka uliopita.

 Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na fununu kwamba Wambui ni mke wa Bw. Kibaki ingawa rais huyo mustaafu aliwahi kukanusha hadharani madai hayo na kusisitiza kwamba anaye mke mmoja tu ambaye ni Bi. Lucy Kibaki.

0 comments:

Post a Comment