Feb 14, 2014

Abul-Futuh: Wamisri watasimama tena kwa mapinduzi

Dk Abdel Moneim Aboul Fotouh mpinzani mashuhuri wa serikali ya hivi sasa nchini Misri ameonya kuwa, wananchi wa nchi hiyo watasimama tena kwa mara nyingine dhidi ya serikali. 

Aboul Fatouh aliyekuwa mgombea wa urais nchini Misri ameongeza kuwa, wananchi wa nchi hiyo watasimama na kuuondoa madarakani utawala wa sasa ambao umekwisha tekeleza jinai nyingi dhidi ya binaadamu na pia kutokana na hali ngumu ya maisha. 

Aidha mwanasiasa huyo ambaye ni mmoja wa viongozi wa zamani wa Harakati ya Ikhwanul-Muslimin amesema kuwa, ukandamizaji unaoshuhudiwa nchini Misri umeongezeka mara kumi zaidi kushinda kipindi cha dikteta Hosni Mubarak rais wa zamani wa taifa hilo. 

Amesisitiza kuwa vikosi vya Mubarak vimerejea tena katika ulingo wa siasa kwa lengo la kulipiza kisasi na vinafanya njama za kuutokomeza uhuru wa wananchi uliopatikana mwaka 2011 kwa kuung’oa madarakani utawala wa dikteta huyo na ili waendeleze ufisadi wao wa muda mrefu. 

Aboul Fatouh amesema kuwa, kile kinachojiri hivi sasa nchini humo, ni hatua dhidi ya mapinduzi na misukosuko ya kupanda na kushuka kwa mapinduzi hayo na kwamba, mapinduzi ya kweli ya wananchi yataibuka tena.

0 comments:

Post a Comment