Serikali ya jimbo la Borno
lililoko Kaskazini mwa Nigeria, inasema kuwa watu 39 wameuawa katika
shambulizi lililofanywa katika mji wa Konduga.
Wanamgambo kadhaa waliokuwa wamejihami kwa bunduki waliingia mji wa Konduga kwa kutumia magari makubwa makubwa.
Watu wengi wameukimbia mji wa Konduga, uliopo kilometa zipatazo ishirini na tano kutoka Maiduguri mji mkuu wa jimbo la Borno Maiduguri.
Wanamgambo wa Kiislam wa Boko Haram, wanaofahamika kwa kuendesha harakati zao katika maeneo hayo wamelaumiwa kwa shambulio hilo.
Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo, wanajeshi wa serikali walioko mjini humo, walishindwa kuwathibiti waasi hao hali iliyowalazimu kutoroka.
Watu wapigwa risasi kiholela
Wanamgambo hao wa Kiislamu, waliwapiga risasi watu hamsini na kuteketeza nyumba kadhaa na pia kuna ripoti kuwa waliwateka nyara wasichana wapatao ishirini kutoka kwa chuo kimoja, kilichoko katika eneo hilo.Wakiongea wakati walipofanya kikao na gavana wa jimbo hilo, raia hao waliokuwa na wasi wasi, walihoji kwa nini maafisa wa ulinzi walichukua muda mrefu kufika eneo hilo baada ya shambulio hilo.
Katika miezi ya hivi karibuni kumekuwa na mashambulio kadhaa katika maeneo ya mashambani, Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo, yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu mia moja.
Mwezi uliopita rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, aliwafuta kazi maafisa wote wakuu wa jeshi, akiwatuhumu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ili kuzuia mashambulio hayo.
Kundi la Boko Haram linaonekana kuwa na wakati zaidi wa kufanya mashambulio katika maeneo kadhaa nchini Nigeria, mashambulio ambayo jeshi la nchi hiyo limekisiwa kushindwa kuyazuia.
0 comments:
Post a Comment