Feb 13, 2014

'Iran iko tayari kwa vita na Marekani, Israel'

Meja Jenerali Hassan Firouzabadi Meja Jenerali Hassan Firouzabadi
Mkuu wa Vikosi Vyote vya Majeshi ya Iran amepuuzilia mbali vitisho vya Marekani kuhusu kuishambulia kijeshi Iran na kusema Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kwa vita vya kuamua mshindi na mshindwa baina yake na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Akizungumza leo Jumatano, Meja Jenerali Hassan Firouzabadi amesema Iran imekuwa ikijitayarisha kwa vita hivyo kwa miaka kadhaa sasa na kwamba Vikosi vya Jeshi la Iran viko tayari kukabiliana vilivyo na hujuma yoyote ile ya kijeshi. 

Kamanda huyo wa ngazi za juu ameonya kuwa, iwapo Iran itashambuliwa, basi maslahi yote ya Marekani na Israel yatalengwa.

Meja Jenerali Firouzabadi amesema kuwa Iran haina uhasama na nchi yoyote ya kanda hii lakini ameongeza kuwa, iwapo Marekani itatumia vituo vyake vya kijeshi katika nchi za eneo hili kuishambulia Iran, basi Iran haitakuwa na budi ila kulenga vituo hivyo.

Kamanda huyo mwandamizi wa jeshi la Iran ametoa tamko hilo kama jibu kwa matamshi ya wakuu wa Marekani ambao katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakisema kuwa 'machaguo yote yako juu ya meza' likiwemo chaguo la kutumia nguvu za jeshi katika kukabiliana na Iran.

0 comments:

Post a Comment