Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) Mkoa wa Singida imewapandisha kizimbani wafanyabiashara
wanne wa Mjini Singida kwa makosa mbalimbali, ikiwemo kutotumia kwa
makusudi mashine za kielekroniki (EFD) kukusanyia kodi, huku wakijua
wazi ni kosa kisheria.
Shtaka lingine linalowakabili wafanyabiashara hao
akiwemo Sabra Mohammed na Khalfani Juma ni kushindwa kulipa kodi ya VAT
kwa makusudi, katika vipindi tofauti kati ya Februari mwaka jana na
Januari mwaka huu, jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya TRA, kifungu
namba 148 cha mwaka 2008.
Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa
Singida Joyce Minde, ilidaiwa na Afisa Sheria Mwandamizi wa TRA Kanda ya
Kaskazini Geva Masele kuwa, wakati washtakiwa wakiendelea na biashara
zao katika eneo la Barabara ya Karume Mjini Singida, walifanya makosa
hayo na hivyo kuikosesha Serikali mapato.
Hata hivyo washtakiwa wote walikana mashitaka yao
na wapo nje kwa dhamana ya Sh2 milioni kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja
na shauri hilo litatajwa tena februari 26 mwaka huu.
Wakati huohuo Robert Mkoma anayefanya biashara
katika Barabara ya Lumumba, Singida amefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi
Wilaya Singida Flora Ndale kwa mashtaka ya kushindwa kulipa kodi na
kutotumia mashine ya kielekroniki (EFD) kwa makusudi, jambo ambalo ni
kosa kisheria.
Katika shauri lingine, TRA imempandisha kizimbani
Rufina Kundya mbele ya hakimu Asha Mwetindwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Mjini Singida kwa kosa la kushindwa kulipa kodi na kutotumia kwa
makusudi mashine ya kieletroniki (EFD), hali ambayo anaikosesha serikali
mapato.
0 comments:
Post a Comment