Feb 19, 2014

Serikali ya CAR yaonya kuhusu upungufu wa chakula

Waziri Mshauri wa Ustawi na Kilimo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, ameonya juu ya upungufu wa chakula unaoikabili nchi hiyo. 

Marie Noƫlle Koyara amesema kuwa, ikiwa vitendo vya ukatili vinavyofanywa na wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka havitakomeshwa haraka, basi nchi hiyo itakumbwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Koyara ameyasema hayo alipofanyiwa mahojiano na waandishi wa habari akiwa ofisini kwake mjini Bangui na kuongeza kuwa, wakulima wachache ndio waliovuna mazao huku wengine wakishindwa kuvuna mazao yao kutokana na machafuko. 

Ameongeza kuwa, kuendelea machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, kuna maana ya kuwafanya wakulima kuikimbia nchi na kusimama shughuli zote za kilimo. 

Waziri wa Ustawi na Kilimo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema kuwa, kabla ya kuzuka kwa mgogoro unaoendelea nchini humo, kulikuwa kukizalishwa mazao mengi yaliyokuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji ya wananchi. 

Lakini hii leo raia wengi wa nchi hiyo hivi sasa wanahitaji chakula kutoka Shirika la Chakula na Kilimo Duniani FAO ili kujikimu kimaisha.

0 comments:

Post a Comment