Feb 19, 2014

Iran yatoa wito kwa nchi za Kiislamu kuungana

Rais Hassan Rouhani Rais Hassan Rouhani
Rais Hassan Rouhani wa Iran ametoa wito kwa nchi za Kiislamu kudumisha umoja ili kuweza kukabiliana na vitisho visivyo na kifani.

 Akihutubia kikao cha ufunguzi wa Mkutano wa Tisa wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu (IIPU) mjini Tehran hii leo, Rais Rouhani amesema, ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa unakabiliwa na mashinikizo na vitisho vya kimataifa. 

Aidha ameonya kuwa vitisho hivyo vya pande zote vitawaathiri Waislamu wote duniani kwa muda mrefu iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa. 

Rais Rouhani amesema Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeidhinisha azimio lililopendekezwa na Iran kuhusu namna dunia inavyoweza kukabiliana na utumiaji mabavu na misimamo mikali. 

Rais wa Iran pia ameashiria matatizo ya wakimbizi wa Syria na mashambulizi ya Israel dhidi ya Wapalestina na kusema, ulimwengu wa Kiislamu unahitaji umoja ili kukabiliana na changamoto hizo. 

 Rouhani aidha amesema, utawala wa Kizayuni wa Israel unafaidika zaidi ya wote kutokana na migogoro katika ulimwengu wa Kiislamu. 

Rouhani amelaani utumizi wa mabavu dhidi ya Waislamu kwa jina la kupambana na ugaidi.

 Rais wa Iran ametoa wito kwa nchi za Waislamu kutelekeza mafundisho ya Kiislamu ili wafanikiwe katika kukabiliana na matatizo yanayowakabili. 

Rouhani ameelezea matumaini yake kuwa kikao cha mabunge ya Kiislamu cha Tehran kitakuwa fursa ya kuimarisha ushirikiano wa nchi za Kiislamu. 

Mkutano huo wa siku mbili unatarajiwa kujadili kwa kina njia za kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu.

0 comments:

Post a Comment